MC Jessy alenga kuingia bungeni 2022

Muhtasari

•Jessy ametangaza atakuwa kwenye kinyang'anyiro cha kiti cha ubunge cha eneo la Imenti Kusini, kaunti ya Meru.

•Wasanii na watu wengine mashuhuri ambao wanamezea viti vya ubunge ni pamoja na Felix Odiwour (Jalang'o)-Lang'ata, MacDonald Mariga-Kibra, Authur Mandela (Xtian Dela)- Westlands, Jackson Ngechu Makini (Prezzo)- Kibra kati ya wengine wengi.

MC Jessy akutana na wazee kutoka South Imenti wikendi iliyopita
MC Jessy akutana na wazee kutoka South Imenti wikendi iliyopita
Image: INSTAGRAM// MC JESSY

Huku kampeni za chaguzi za mwaka wa 2022 zikiwa zimeanza kunoga kote nchini wagombeaji wapya wa viti mbalimbali  wameendelea kujitokeza.

Wasanii na watu mashuhuri wengi wameonekana kumezea mate viti mbalimbali vya kisiasa huku wengine tayari wakiwa wametangaza azma yao.

Msanii wa hivi karibuni kutangaza kujiunga nia yake ya kuwania kiti mwaka ujao ni mchekeshaji Jasper Muthomi almaarufu kama MC Jessy.

Kupitia mitandao yake ya kijamii, Jessy ametangaza atakuwa kwenye kinyang'anyiro cha kiti cha ubunge cha eneo la Imenti Kusini, kaunti ya Meru.

Wikendi  iliyopita msanii huyo wa Churchill Show alipokea wazee kutoka eneo bunge la Imenti Kusini ambao walimpa baraka anapotazamia kuanza kampeni zake.

"Wanasema ambacho wazee wanaona  wakiwa wameketi, wanaume wadogo wataweza kuona tu wakiwa wamekantanga mabega yao. Mimi ni mwanafunzi wa theolojia na naamini kwamba darasa nzuri zaidi ni kwenye miguu ya wazee. Wikendi iliyopita nilifurahia kupokea wazee ambao walinilea na ambao wametoka kutoka eneo bunge langu South Imenti na wakanipa baraka na majukumu ya kuongoza Imenti Kusini" Jessy alisema.

Jessy anatazamia kumbandua Kathuri Murungi ambaye sasa amekalia kiti hicho kwa muhula wa pili mfulululizo.

Wasanii na watu wengine mashuhuri ambao wanamezea viti vya ubunge ni pamoja na Felix Odiwour (Jalang'o)-Lang'ata, MacDonald Mariga-Kibra, Authur Mandela (Xtian Dela)- Westlands, Jackson Ngechu Makini (Prezzo)- Kibra kati ya wengine wengi.