Wanawe Esther Musila wafunguka kuhusu uhusiano wao na baba yao wa kambo, Guardian Angel

baba yao mzazi alifariki takriban miaka mitano iliyopita.

Muhtasari

•Gilda Musila na Glen Musila walisema walimpokea Guardian Angel vizuri alipojiunga na familia yao.

•Gilda alisema alimpenda sana baba yao marehemu huku akieleza kuwa Guardian Angel alipojiunga na familia alielewa kwamba hawakuhitaji baba mwingine.

•Glen alisema wanaelewana vizuri na mwanamuziki huyo wa nyimbo za injili kuona kuwa angali kijana bado

Image: INSTAGRAM// GUARDIAN ANGEL

Watoto wa Bi Esther Musila wamefunguka kuhusu uhusiano wao na baba wao wa Kambo mwanamuziki Peter Omwaka almaarufu kama Guardian Angel.

Walipokuwa kwenye mahojiano na Mungai Eve wakati wa hafla ya kuzindua albamu mpya ya mwanamuziki huyo siku ya Jumamosi, Gilda Naibei Musila na Glen Musila walisema walimpokea Guardian Angel vizuri alipojiunga na familia yao.

Wawili hao walisema waliridhishwa na namna msanii huyo alijiunga na familia yao huku wakieleza kwamba hakujitambulisha kama baba wa kambo ila kama rafiki.

"Yeye ni kama mshauri. Yeye ni rafiki. Hatuwezi sema yeye ni kama baba, anajaribu kuwa baba. Sababu moja tulielewana vizuri na yeye ni kwa sababu hakuja na fujo akisema eti atakuwa bab wetu wa kambo na kuharibu kila kitu. Alikuja kama rafiki na kusema tunaweza zungumza naye kuhusu kitu chochote" Gilda alisema.

Mwanadada huyo aliweka wazi kwamba baba yao mzazi alifariki takriban miaka mitano iliyopita. 

Alisema walimpenda sana baba yao marehemu huku akieleza kuwa Guardian Angel alipojiunga na familia alielewa kwamba hawakuhitaji baba mwingine.

"Tulikuwa na baba, tuko na baba. Alikuwa anaitwa Erick, roho yake ipumzike kwa amani. Alikuwa baba mzuri, tulimpenda. Tulimpoteza 2016. Naweza sema niko na baba. Guardian sana sana ni kama mshauri" Gilda alisema.

Glen alisema wanaelewana vizuri na mwanamuziki huyo wa nyimbo za injili kuona kuwa angali kijana bado.

Alisema alikubali hali ilivyokuwa baada ya kuona ni wazi kuwa mama yake na Guardian Angel ni wanandoa wa kweli.

"Nilijizoesha  kwa sababu nilikuja kuona ni kitu halisi. Kitu kizuri kwake ni kizuri kwetu pia. Nilikubali na hicho ndicho kitu muhimu ningefanya" Glen alisema.

Gilda aliongeza kuwa Guardian Angel huwa anawashika mkono sana katika mambo mbalimbali maishani.

"Guardian Angel huwa anatuunga mkono. Huwa anatusaidia kwa namna kubwa sana. Kwa njia zote huwa anaonyesha usaidizi" Gilda alisema.

Bi Musila na Guardian Angel walianza kuchumbiana mwaka uliopita baada ya kujuana kupitia mtangazaji Maina Kageni.