"Mlima wote, baba tosha" Ben Githae afanya upya wimbo wake 'Tano tena' kupigia debe Raila Odinga

Muhtasari

•Githae amesema amebadilisha wimbo huo ambao alibuni  takriban miaka mitano iliyopita kupigia debe rais Uhuru Kenyatta ili sasa uweze kutumika katika kampeni za Raila Odinga.

•Amewasihi wakazi wa Pwani wampigie kura kinara wa ODM mwaka ujao huku akidai eneo la Mt Kenya tayari limeamua kuunga mkono azma yake ya kuwania urais kwa mara ya tano.

Image: INSTAGRAM// BEN GITHAE

Mwanamuziki mashuhuri wa nyimbo za injili na kisiasa Ben Githae ameufanya upya wimbo wake 'Tano tena' kuugeuza kuwa wa kupigia debe kinara wa ODM Raila Odinga.

Alipokuwa anatoa hotuba yake katika mkutano wa siasa uliofanyika Kwale asubuhi ya Jumanne, Githae alisema ameamua kubadilisha maneno ya wimbo wake kuona kwamba eneo la mlima Kenya linamuunga mkono kinara wa ODM.

Githae amesema amebadilisha wimbo huo ambao alibuni  takriban miaka mitano iliyopita kupigia debe rais Uhuru Kenyatta ili sasa uweze kutumika katika kampeni za Raila Odinga.

"Mimi ni Ben Githae yule alisema 'Tano tena' na 'Wembe ni ule ule' . Saa hii tumegeuza huo wimbo tunasema 'Ndani ndani ndaniii to the state house, mlima wote baba tosha'" Githae alisema.

Mwanamuziki huyo amewasihi wakazi wa Pwani wampigie kura kinara wa ODM mwaka ujao huku akidai eneo la Mt Kenya tayari limeamua kuunga mkono azma yake ya kuwania urais kwa mara ya tano.

Mwaka wa 2017 wimbo 'Tano tena' ulitumika sana kupigia chama cha Jubilee kampeni. 

Baada ya mahakama kutupilia mbali matokeo ya urais katikachaguzi hizo Githae alitoa wimbo 'Wembe ni ule ule' ambao ulitumika katika kampeni za marudio ya uchaguzi.