"Ulinipa vyeo vizuri" DJ Mo na Size 8 washerehekea siku ya kuzaliwa ya kifungua mimba wao

Muhtasari

•Wanandoa hao wametimiza ombi la binti yao la kupelekewa keki shuleni ili aweze kusherehekea pamoja na marafiki wake.

•Mapema mwezi uliopita  wanandoa hao walimpoteza ambaye angekuwa mtoto wao wa tatu baada ya Size 8 kulazimika kufanyiwa upasuaji wa dharura kufuatia matatizo ya ujauzito.

Pamoja:Size 8 na DJ Mo

Kifungua  mimba wa mcheza santuri Samuel Muraya almaarufu kama DJ Moh namwanamuziki Linet Munyali almaarufu kama Size 8 anaadhimisha siku ya kuzaliwa.

Siku ya leo (Alhamisi) Ladasha Belle Muraya anasherehekea kufikisha miaka sita.

DJ Moh na Size 8 wametumia kurasa zao za mitandao ya kijamii kusherehekea siku ya kuzaliwa ya binti wao.

Wanandoa hao wametimiza ombi la binti yao la kupelekewa keki shuleni ili aweze kusherehekea pamoja na marafiki wake, kama alivyoeleza DJ Moh chini ya video inayoonyesha Ladasha akipuliza mshumaa.

Mo amemsherehekea sana bintiye huku akimshukuru Mola kwa kumtunuku zawadi hiyo ya ajabu.

"Ulinipa vyeo vizuri, Baba/Baba-mwaka wa 2015 … Yaani upendo nilio nao kwako Mungu pekee ndiye anayejua ..tunamshukuru Mungu kwa ajili yako, zawadi nzuri sana .. imekuwa safari nzuri kukuona ukikua. Kama wazazi wako tunajivunia wewe. Mungu akulinde na akupende zaidi ya wazazi wako 😻. Tuko hapa kwa ajili yako. Nisaidieni kumtakia binti yangu heri za kuzaliwa anapofikisha miaka 6" Mo ameandika.

Size 8 amepakia video inayoonyesha akicheza densi na bintiye darasani huku akijiandaa kukata keki.

Mapema mwezi uliopita  wanandoa hao walimpoteza ambaye angekuwa mtoto wao wa tatu baada ya Size 8 kulazimika kufanyiwa upasuaji wa dharura kufuatia matatizo ya ujauzito.