Harmonize ataja sababu zilizochangia mapokezi baridi aliyopata katika ziara yake ya Marekani

Muhtasari

•Harmonize alikiri kwamba ni kweli kulikuwa na changamoto huku akidai ilichangiwa zaidi na kukosa msingi thabiti wa mashabiki na kutoshirikiana kwa wanamuziki wa Afrika Mashariki.

•Konde Boy amewasihi wasanii wa Afrika Mashariki kuiga mfano wa wasanii wa Afrika Magharibi wa kushirikiana zaidi ili  kujenga misingi mizuri ya Mashabiki Ughaibuni.

•Harmonize pia alisema kuna mgawanyiko mkubwa wa mashabiki Ughaibuni ambao wameapa kuhudhuria shoo za wasanii wanaoshabikia tu.

Image: INSTAGRAM// HARMONIZE

Siku chache zilizopita staa wa Bongo Rajab Abdul Kahali almaarufu kama Harmonize alitamatisha ziara yake ya kimuziki ya  miezi mitatu nchini Marekani.

Harmonize alirejea Tanzania siku ya Alhamisi na kupokewa na  baadhi ya mashabiki pamoja na waandishi wa habari katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere.

Alipokuwa anahojiwa na wanahabari, Harmonize alizungumza kuhusu mapokezi ambayo alipata Marekani.

"Mapokezi yalikuwa ni mazuri. Kama mlivyoona kila shoo ilikuwa na nafasi yake .Kuna shoo ambazo ziliandaliwa kama Harmonize headliner. Kuna pia special appearance na tamasha ambazo nilifanya. Mapokezi  yalikuwa ni mazuri" Harmonize aliema.

Uvumi ulikuwa umetanda kote mitandaoni kwamba mwanamuziki huyo mzaliwa wa Mtwara, Tanzania hakupata mapokezi mazuri kama alivyotarajia.

Harmonize alikiri kwamba ni kweli kulikuwa na changamoto huku akidai ilichangiwa zaidi na kukosa msingi thabiti wa mashabiki na kutoshirikiana kwa wanamuziki wa Afrika Mashariki.

"Changamoto kwetu kama wasanii wa Afrika Mashariki, ukitangaza shoo kama Harmonize watakaokuja pale ni mashabiki wa Harmonize tu sio mashabiki wa mtu mwingine. Nimejifunza tunatakiwa tuwe kitu kimoja kama Afrika Mashariki. Kuwa kitu kimoja ni pamoja na kushirikiana. Kwa mfano watu waone Harmonize na Eddy Kenzo, Harmonize na Bruce Melody pamoja. Kwetu sisi wakisema eti hatujapata watu wengi, kusema kweli wingi wa watu kwa shoo ambazo nilikuwa nafanya huwezi nilinganisha na Wizkid, Burnaboy na wengine. Wenzetu wanakuwa soldout kwa tamasha. Wanafanya shoo siku ya kwanza, ya pili kwa sababu washatengeneza hiyo misingi kitambo na pia ushirikiano wao ni mzuri" Alisema Harmonize.

Konde Boy amewasihi wasanii wa Afrika Mashariki kuiga mfano wa wasanii wa Afrika Magharibi wa kushirikiana zaidi ili  kujenga misingi mizuri ya Mashabiki Ughaibuni.

"Hatujachelewa. Nadhani bado tuna nafasi. Kwa hilo suala la ushirikiano sio kwa wasanii tu. Ni suala ambalo linahitaji watu wote kama vile wadau, mapromoters. Mapromoters wengi wa Afrika Mashariki hawafanyi kazi kwa ushirikiano kama vile tu wasanii. Unaweza pata promoter wa Kenya ni Kenya. Akitangaza shoo capacity yake inakuwa ni Kenya tu" Harmonize alisema.

Harmonize pia alisema kuna mgawanyiko mkubwa wa mashabiki Ughaibuni ambao wameapa kuhudhuria shoo za wasanii wanaoshabikia tu.

Hata hivyo alisema amejifunza mambo mengi katika ziara yake ya Marekani na anatarajia kuyafanyia kazi ili kupata mafanikio zaidi wakati mwingine.