"Nilipoambiwa amefariki nilianguka chini nikalia" Size 8 asimulia masaibu aliyopitia wakati alipoteza mtoto wake

Muhtasari

• Size 8 alisema aliishiwa nguvu  na kuangua kilio kikubwa wakati alifahamishwa kuhusu kifo cha mtoto wake tumboni.

• Alisema baada ya kujifungia katika chumba chake na kuomba kwa kipindi kirefu alikubali yaliyokuwa yametendeka na kuomba Maulana aweke maisha yake salama kwa ajili ya watoto wake.

• Kulingana na Size 8, kitendo cha Yesu kusulubiwa msalabani kwa sababu ya dhambi za wanadamu ni cha thamani zaidi kuliko mtoto wake na mumewe.

Image: INSTAGRAM// SIZE 8

Mwanamuziki wa nyimbo za injili Linet Munyali almaarufu Size 8 amefunguka kuhusu yale aliyopitia wakati alipoteza mtoto wake kabla ya kuzaliwa mapema mwezi uliopita.

Akiwa kwenye mahojiano  na Chris Baraka hivi majuzi, Size 8 alisema aliishiwa nguvu  na kuangua kilio kikubwa wakati alifahamishwa kuhusu kifo cha mtoto wake akiwa tumboni.

Mke huyo wa mcheza santuri Samuel Muraya almaarufu DJ Moh alisema wauguzi walimfahamisha kuwa maisha yake yalikuwa hatarini kutokana na shinikizo la damu.

"Nilipoambiwa eti moyo wa mtoto haudundi, nilianguka chini nikalia. Nililia, nikalia sana. Nilikuwa hata nashikiliwa na muuguzi. Waliniambia eti maisha yangu ndiyo yalikuwa hatarini juu ya shinikizo la damu" Alisema Size 8.

Baada ya kupoteza mtoto wake Size 8 aliomba aruhusiwe kuenda nyumbani ambako aliendeleza kilio huku akipiga sala kwa Mungu ili kuomba nguvu za kukabiliana na majonzi.

Alisema baada ya kujifungia katika chumba chake na kuomba kwa kipindi kirefu alikubali yaliyokuwa yametendeka na kuomba Maulana aweke maisha yake salama kwa ajili ya watoto wake.

"Nilijifungia kwa nyumba, nikalia mbele ya Mungu na baada ya hapo nikamwambia ni sawa. Nilimuomba Mungu aweke maisha yangu salama kwa ajili ya watoto wangu.  Hiyo siku ata sikulala na bwanangu. Nililala na watoto wangu. Niliwakumbatia usiku wote nikiomba Mungu aniruhusu niendelee kuishi kwa ajili ya watoto wangu na nikaahidi kumpa maisha yangu afanye atakavyo" Alisimulia Size 8.

Alisema baada ya kuomba na kulia usiku kucha huku akiwa amekumbatia watoto wake alipokea neema ya Mungu ambayo ilifuta machozi yake.

Size 8 alifichua kwamba angewazuia watu kumwona kwa kuwa walitarajia awe anaomboleza ilhali majonzi yake tayari yalikuwa yameisha.

"Mungu alinipa raha na amani kutokana na ufunuo kuwa shetani angeweza kuja anitese kwa namna yoyote ila hawezi chukua upendo na ufahamu wa Mungu" Alisema Size 8.

Mwanauziki huyo alisema anaamini wakati utafika ambapo masaibu ambayo yalimkumba yatageuka kuwa neema.

"Najua tukio langu kupoteza mtoto imebadilika kuwa nzuri kwangu" Size 8 alisema

Kulingana na Size 8, kitendo cha Yesu kusulubiwa msalabani kwa sababu ya dhambi za wanadamu ni cha thamani zaidi kuliko mtoto wake na mumewe.