Aliyekuwa gavana wa Nairobi Mike Sonko amezidi kumpongeza mhubiri mashuhuri Lucy Natasha kufuatia hatua ya kuvishwa pete ya uchumba na mpenzi wake Stanley Carmel.
Sonko ametumia kurasa zake za mitandao ya kijamii kumtakia mhubiri huyo wake ndoa yenye furaha na kumuombea abarikiwe na watoto wengi.
Mwanasiasa huyo ambaye amekuwa akivuma sana siku za hivi majuzi kufuatia video tatanishi alizovunjisha mitandaoni amepuuzilia mbali madai kuwa pia ako na video za mhubiri huyo ambazo atakuwa anavunjisha hivi karibuni.
"Huwa vizuri kuwa na mhubiri ambaye anakuombea. Hii mambo ati kuna video za Rev Natasha ni upuzi mtupu na ikemewe kabisa. Tunakutakia ndoa yenye furaha na watoto wengi wa Mungu. Kazi ya MC Siku ya harusi sijakataa" Sonko aliandika.
Natasha alivishwa pete ya uchumba na Carmel siku ya Jumamosi katika hafla ya kufana iliyoandaliwa katika hoteli ya boma jijini Nairobi.
"Nimesema ndio!" Natasha aliandika kwenye ukurasa wake wa Facebook alipokuwa anatangaza hatua hiyo mpya maishani mwake.
Aliombea ndoa yake neema tele, baraka, ulinzi na mwongozo mzuri.
Mamia ya Wakenya wameendelea kumpongeza mchungaji huyo kwa hatua aliyopiga huku wakimtakia mema katika ndoa.