"Hatungeweza kumudu jeneza la mama yetu!" MC Jessy asimulia alivyopoteza wazazi akiwa mdogo sana

Muhtasari

•Jessy alisema babake ndiye alitangulia kuaga akiwa mchanga mno, hata kabla hawajapata kufahamiana vizuri.

•Mamake Jessy aliangamizwa na ugonjwa wa Malaria siku ambayo alikuwa anafanya mazoezi ya mtihani wa KCPE.

•Licha ya mama yake kufa siku moja tu kabla ya mitihani yake kung'oa nanga, Jessy aliendelea kufanya karatasi zote na mazishi yakafanyika alipokamilisha.

MC Jessy na Massawe Japanni katika studio za Radio Jambo
MC Jessy na Massawe Japanni katika studio za Radio Jambo
Image: RADIO JAMBO

Mchekeshaji mashuhuri Jasper Muthomi almaarufu kama MC Jessy amefunguka kuhusu maisha yake magumu ya utotoni.

Akiwa kwenye mahojiano na Daniel 'Churchill' Ndambuki, mchekeshaji huyo alifichua kwamba alipoteza wazazi wake wawili akiwa na umri mdogo sana.

Jessy alisema babake ndiye alitangulia kuaga akiwa mchanga mno, hata kabla hawajapata kufahamiana vizuri.

"Babangu aliaga nikiwa mdogo sana. Hata hatukuwa tumepata uhusiano mkubwa eti ningeishi kumjua. Aliaga alafu nikaishi na mama yangu. Alinilea kama single mother. Mimi ni zao la maarifa ya mwanamke" Jessy alisimulia.

Mchekeshaji huyo ambaye analenga kuingia bungeni mwaka ujao alisema mama yake alifanya kazi ya kuuza mbao ili aweze kumudu malezi yao.

Kwa bahati mbaya mamake Jessy aliangamizwa na ugonjwa wa Malaria siku ambayo alikuwa anafanya mazoezi ya mtihani wa KCPE. Wakati huo alikuwa na umri wa miaka 12.

"Mama yangu alipokuwa anatulea alipata kazi ya kuuza mbao Embu. Tulienda pale nikasoma darasa la sita, saba na la nane. Tukimaliza darasa la nane, ilikuwa siku ya rehearsals. Niliacha mamangu akiwa mgonjwa, alikuwa amepatikana na Malaria. Nilikuwa mgonjwa kwa hivyo niliambiwa tu kwamba ni mgonjwa. Nilimuacha nyumbani kama amelala kidogo nikaenda rehearsals. Ilikuwa siku ya Jumatatu, KCPE ilikuwa Jumanne. Tulitoka rehearsals nikaenda nyumbani nikasikia watu wanaimba kwa umbali. Aliaga siku hiyo nikifanya rehearsals za KCPE" Alisimulia.

Jessy alikiri kwamba wakati  alimpoteza mamake ndicho kipindi kigumu zaidi amewahi kupitia katika maisha yake. 

Licha ya mama yake kufa siku moja tu kabla ya mitihani yake kung'oa nanga, Jessy aliendelea kufanya karatasi zote na mazishi yakafanyika alipokamilisha.

"Hakuna mtu aliyeniambia, nilihisi tu amefariki. Mtu unayempenda anapoaga, utaihisi moyoni  kwa sababu mlikuwa mmeungana sana. Mama yangu ndiye alikuwa rafiki wangu wa dhati. Vile alienda yeye ndiye alikuwa mzazi wa mwisho niliyekuwa naye. Siku iliyofuata niliamka na nikaenda nikafanya mitihani yangu, tulimaliza Alhamisi. Siku ya Ijumaa tukaenda Meru, tukamzika Jumamosi. Hiyo Ijumaa ata tukiwa Meru, hatungeweza kumudu hata jeneza la mama yangu. Saa ile alizikwa watu wakaenda" Alisema.

Mchekeshaji huyo alisema nyanya na babu yake ndio walichukua jukumu la kumlea kufuatia kifo cha wazazi wake wawili.

Alisema jambo la kupoteza wazazi wote wawili na kuachwa yatima lilimtia huzuni kubwa moyoni.