'Nawaonea wivu malaika juu wanakuona kila siku,' Willis Raburu amkumbuka marehemu bintiye kwa ujumbe wa kihisia

Muhtasari

β€’Raburu amekiri kwamba tangu Adana alipoaga huwa anapatwa na mchanganyiko wa hisia kila mwisho wa mwaka  kwani hajui ikiwa anapaswa kusherehekea mwanzo wa mwaka mpya ama kuomboleza bintiye.

Image: INSTAGRAM// WILLIS RABURU

Mburudishaji na mtangazaji maarufu wa Citizen TV Willis Raburu amemkumbuka marehemu binti yake takriban miaka miwili baada yake kuaga.

Katika ukurasa wake wa Instagram Raburu amemnakilia bintiye Adana ujumbe maalum wa kihisia akiadhimisha siku ambayo marehemu alizaliwa.

Katika ujumbe wake Raburu amesema anatamani sana  angekuwa anasherehekea birthday ya pili ya bintiye pamoja naye huku akiongeza kwamba kwa kuwa sasa hayupo tena amebaki kuwaonea wivu malaika wa mbinguni ambao wanapata kumuona kila siku.

"Heri ya miaka 2 ya kuzaliwa Adana. Malaika wangu. Ninakufikiria kila wakati ninao. Ninakukumbuka na uso wako mzuri. Sitasahau kwani muda ule nilikuwa nawe katika chumba baridi na hata busu langu halingeweza kukurudisha hai! Nadhani hiyo inafanyika katika hadithi za hadithi tu. πŸ˜”πŸ’” Nilipaswa kuwa nikisherehekea hatua zako muhimu lakini badala yake nimekaa hapa nikionea malaika wivu kwa sababu wanapata kuwa nawe kila siku." Raburu aliandika.

Amekiri kwamba tangu Adana alipoaga huwa anapatwa na mchanganyiko wa hisia kila mwisho wa mwaka  kwani hajui ikiwa anapaswa kusherehekea mwanzo wa mwaka mpya ama kuomboleza bintiye.

"Siku zote  kama hii ni siku ngumu kwa sababu sijui kusherehekea mwaka mpya au kuomboleza. Najua ungetaka tukusherehekee na ndio maana niko hapa. Piga kelele nyingi mbinguni leo wajulishe wazazi wako ni akina nani! 😒 Nakupenda. Mama na baba watakupenda milele na milele! πŸ™πŸΎπŸ’”β€οΈπŸ˜‡" Aliandika Raburu.

Binti ya mtangazaji huyo alifariki wakati aliyekuwa mke wake Marya Prudence alikuwa anajifungua mnamo Desemba 31, 2019.