"Haina haja kujiona mwamba eti unajua kila kitu!" Harmonize awasihi wasanii wa Afrika Mashariki kushirikiana

Muhtasari

•Harmonize alisema alipokuwa katika ziara yake ya muziki Marekani aligundua kuwa umaarufu ambao wasanii hujiona wakiwa nao hapa Afrika Mashiriki huisha wanapoenda kutumbuiza nje. 

•Pia aliwahimiza wenzake kutia bidii zaidi katika muziki wao huku akiwatahadharisha dhidi ya kutumia njia haramu za kutafuta sifa kama vile kununua 'views'

Harmonize na Alikiba
Harmonize na Alikiba
Image: INSTAGRAM

Mwanamuziki mashuhuri wa Bongo Rajab Abdul Kahali almaarufu kama Harmonize ametoa wito kwa wasanii wote wa Afrika Mashariki haswa kutoka Tanzania kuwa na ushirikiano mzuri.

Alipokuwa anazungumza katika tamasha ya kusikiliza Albamu yake mpya 'High School' iliyofanyika mkesha wa mwaka mpya, Harmonize alikiri alipokuwa katika ziara yake ya muziki Marekani alijifunza kuwa umaarufu ambao wasanii hujiona  kuwa nao hapa Afrika Mashiriki huisha wanapoenda kutumbuiza nje. 

Staa huyo wa Bongo aliwaomba wanamuziki wenzake wasije wakajipiga kifua na kujiona bora zaidi kuliko wengine na badala yake washirikiane kuinua muziki wa Afrika Mashariki.

"Ziara yangu ya Marekani ilinifunza mambo mengi sana. Hakuna haja ya kulifanya pekee yako. Haina haja ya kujiona wewe ni mwamba unajua kila kitu. Sisi ni Watanzania, sisi ni Waafrika Mashariki. Tuungane tupeleke muziki wetu kwenye kiwango cha juu. Tukiwa hapa ndani tunakuwa wakubwa lakini tukitoka nje inakuwa kitu tofauti. Hakuna anayeweza kudanganya" Harmonize alisema.

Konde Boy alisema mwaka huu wa 2022 angependa kuona wasanii wakishirikiana zaidi na kuinuana. 

Pia aliwahimiza wenzake kutia bidii zaidi katika muziki wao huku akiwatahadharisha dhidi ya kutumia njia haramu za kutafuta sifa kama vile kununua 'views'

"Mwaka wa 2022 ningependa kuona hamna msanii ambaye ananunua viewers. Wote tufanye kazi kwa bidii tuweze kusonga mbele kwa ushirikiano. Jambo hilo mzee tunatupa 2021" Alisema Harmonize.

Mwaka uliopita Harmonize alifanya ziara ya muziki ya miezi mitatu Marekani.

Baada ya kurejea Tanzania Harmonize alikiri kwamba ziara yake ilikabiliwa na changamoto kadhaa huku akieleza kuwa ilichangiwa zaidi na kukosa msingi thabiti wa mashabiki na kutoshirikiana kwa wanamuziki wa Afrika Mashariki.