Khadija Kopa azungumzia mahusiano ya binti yake Zuchu, akiri hamna tatizo iwapo ataolewa kama mke wa pili

Muhtasari

•Bi Kopa alisema atakuwa radhi iwapo hatima ya binti yake itakuwa kuolewa kwa boma ambalo tayari lina wake wengine kwani dini yao ya Kiislamu inawaruhusu wanaume kuwa na hadi wake wanne.

•Kopa alisema mahusiano ya Zuchu na Kiba yalipotamatika bintiye aliamua kuendelea na maisha yake na kufikia sasa hajawahi kumtambulisha mume mwingine.

Khadija Kopa, Zuchu
Khadija Kopa, Zuchu
Image: HISANI

Nguli wa muziki wa Taarab  Khadija Omar Abdallah Kopa almaarufu kama Khadija Kopa ameapa hatakuwa na upinzani wowote iwapo  binti yake Zuhura Othman Soud almaarufu kama Zuchu ataja kuolewa nyumba ndogo.

Alipokuwa kwenye mahojiano ya hivi majuzi na Mbengo TV, mtunzi huyo wa nyimbo kutoka Zanzibar alisema atakuwa radhi iwapo hatima ya binti yake itakuwa kuolewa kwa boma ambalo tayari lina wake wengine kwani dini yao ya Kiislamu inawaruhusu wanaume kuwa na hadi wake wanne.

Kopa alisema cha muhimu zaidi ni binti yake awe na raha katika ndoa yake na mumewe aje kumpenda  vizuri bila kumpa shida zozote.

"Sisi ni Waislamu. Mwanamume atake wanawake watatu na yeye wa nne, hamna taabu. Mradi yeye mwenyewe akiridhia, sisi ni Waislamu na tunatakiwa turidhie. Wanaume ni watu wengine tofauti, hawaridhiki kwa mwanamke mmoja. Hiyo ndiyo tabia yao. Ni heri awe na ndoa kuliko kuzidi. Kwetu haina shida, ata yeye haimpi taabu kwa sababu sisi tumetokea kwenye misingi ya Kiislamu. Bora mumewe ampende, asimpe shida, hampigi na  nini na mwenziwe awepo niko radhi kabisa" Bi Kopa alisema.

Kigogo huyo wa Taarab alisema katika kisiwa anachotokea cha Zanzibar ni kawaida kwa boma moja kuwa na wake zaidi ya mmoja.

Bi Kopa  alifichua kuwa kufikia sasa Zuchu amewahi kutambulisha mwanamume mmoja tu kama mpenzi wake ila mahusiano yao hayakudumu.

"Alishafika huyo Kiba. Alivyokuwa anasoma chuo aliporudi babake alimwambia atakapohitaji kuwa na mtu bora amlete nyumbani ili kama kutakuwa na uelewano wafunge ndoa asije akahangaika. Walivyokutana huko chuo na kusaidiana katika mambo ya masomo alifika nyumbani akamtambulisha. Zuhura alikuja akachukuliwa akapelekwa kwao. Tulikuwa tunajua kwamba wakati wowote ndoa ingekuwa lakini bahati mbaya hawakuwahi" Kopa alisema.

Kopa alisema mahusiano ya Zuchu na Kiba yalipotamatika bintiye aliamua kuendelea na maisha yake na kufikia sasa hajawahi kumtambulisha mume mwingine.