"Tumekaribia kufika, endeleeni kuniombea" Akuku Danger azungumza kuhusu afya yake

Muhtasari

•Akuku amesema anawathamini wote ambao wamekuwa wakimwombea, kumfariji na ambao wamechangia bili yake ya hospitali huku akiwahakikishia kwamba afya yake inaendelea kuimarika.

•Dacha amefichua kwamba mchekeshaji huyo anatarajiwa kuruhusiwa kutoka hospitali mnamo Jumamosi.

Akuku Danger
Akuku Danger
Image: INSTAGRAM

Mchekeshaji wa Churchill Show Mannerson Oduor Ochieng almaarufu kama Akuku Danger amezungumza na wanamitandao kwa mara ya kwanza tangu alipoanza kuugua mwezi uliopita.

Kupitia kanda ya video iliyochapishwa na mwandani wake Sandra Dacha (Silprosa) kwenye mtandao wa Instagram, Akuku Danger amewashukuru wote ambao wamekuwa wakisimama naye katika kipindi hiki kigumu maishani mwake.

Akuku amesema anawathamini wote ambao wamekuwa wakimwombea, kumfariji na ambao wamechangia bili yake ya hospitali huku akiwahakikishia kwamba afya yake inaendelea kuimarika.

"Shukran kila mtu kwa kuonyesha upendo, kwa usaidizi wenu na maombi. Kwa wale ambao wameonyesha upendo, kwa waliochangia bili ya hospitali na wanaoendelea kuchanga nawashukuru sana kutoka moyoni mwangu. Tunakaribia kufika pale , endeleeni kuniombea na nawathamini nyote" Akuku amesema.

Dacha amefichua kwamba mchekeshaji huyo anatarajiwa kuruhusiwa kutoka hospitali mnamo Jumamosi.

Amewasihi Wakenya kuendelea kuchangia bili ya hospitali ya Akuku ili kumwezesha kuachiliwa  kwenda nyumbani.

"Tafadhali tusaidieni kupeleka Akuku Danger nyumbani, tafadhali. Ataruhusiwa kwenda nyumbani kesho. Paybill 891300 ACC (Weka jina lako)" Dacha amesema kupitia ukurasa wake wa Instagram

Wanamitandao wameendelea kumtakia mchekeshaji huyo afueni ya haraka.