Hamisa Mobetto asherehekea siku ya kuzaliwa ya Rick Ross kwa ujumbe mtamu

Muhtasari

•Rapa huyo mzaliwa wa Marekani na ambaye anajulikana kuwa na utajiri mkubwa alisherehekea kuhitimu miaka 46.

•Kwa kipindi kirefu uhusiano kati ya wasanii hao umetiliwa shaka huku wengi wakiamini kwamba wawili hao wanachumbiana.

Hamisa Mobetto na Rick Ross
Hamisa Mobetto na Rick Ross
Image: INSTAGRAM

Mnamo Ijumaa mwanamuziki wa nyimbo za kufoka William Leonard Roberts II almaarufu kama Rick Ross aliadhimisha siku yake ya kuzaliwa.

Rapa huyo mzaliwa wa Marekani na ambaye anatambulika kuwa na utajiri mkubwa alisherehekea kuhitimu miaka 46.

Maelfu ya mashabiki wake kutoka kote duniani walimsherehekea na kumwandikia jumbe za kheri za kuzaliwa.

Mwanamuziki na mwigizaji mashuhuri kutoka Bongo Hamisa Mobetto hakusalia nyuma katika kumtakia rapa huyo heri za kuzaliwa huku akimtambulisha kama 'Boo'. Mobetto alimtaja Rick  Ross kama mtu wa ajabu.

"Kwa mwanaume huyu hapa. Shukran kwa kuwa wa ajabu kweli. Heri za siku ya kuzaliwa Boo @richforever" Mobetto alimwandikia Ross siku ya Jumamosi na kuambatanisha na emoji zilizoashiria upendo..

"Sisi ndio wakubwa zaidi" Rick Ross alijibu

Kwa kipindi kirefu uhusiano kati ya wasanii hao umetiliwa shaka huku wengi wakiamini kwamba wawili hao wanachumbiana.

Aghalabu wawili hao wameonekana wakiandikiana jumbe tamu kwenye mitandao ya kijamii na hata walionekana wakijivinjari pamoja jijini Dubai mwaka jana.

Hivi majuzi Mobetto akiwa kwenye mahojiano alisema rapa huyo ni rafiki wake wa karibu na mshirika wake wa kibiashara.

“Sisi ni kama familia kubwa na tumefanya vitu vingi pamoja ambavyo nitakuwa navizindua hivi karibuni’’, Mobetto alisema.

Mlimbwende huyo wa Bongo alisema uhusiano wao ni  kama wa 'kifamilia' kwani wamekuwa wakifanya kazi pamoja kwa muda.

Mpenzi huyo wa zamani wa Diamond Platnumz hakukiri uwepo wa mahusiano ya kimapenzi kati yake na Rick Ross wala kukana huku akiahidi kufahamisha watu hivi karibuni iwapo kuna chochote cha ziada kati yao