Malkia wa Bongo Zuhura Othman almaarufu kama Zuchu amesema kwamba yuko tayari kuanzisha familia.
Akiwa kwenye mahojiano na Wasafi Media, Zuchu alikiri kuwa anampenda sana mpenzi wake wa sasa na yuko tayari kukubali ombi lake la ndoa iwapo atachukua hatua hiyo.
Mtunzi huyo wa kibao 'Sukari' alieleza kwamba atakapokuwa katika ndoa halisi anakusudia kupata angalau watoto wawili.
"Nampenda sana, nampenda kweli. Sasa hivi akisema anataka kuniona nitasema ndio. Niko tayari kuolewa. Ukishakubali kuolewa basi umekubali kuanzisha familia. Nataka kupata watoto wawili" Zuchu alisema.
Mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka 28 pia alisema kuwa hana tatizo lolote na kuwa mama wa kambo kwa kuwa anawapenda sana watoto.
Zuchu alifichua kuwa mahusiano kati yake na mpenziwe ambaye amekuwa akimficha hadharani kwa kipindi kirefu hayakuwa na mwanzo rahisi.
Alisema kazi yake ya usanii iliweka mazingira magumu kwa mahusiano yao kuanza na kukua kwa kasi.
"Ilikuwa ngumu sana kunipata kutokana na nilivyo. Hatukuanzia kwenye mapenzi tu. Ilianza na yeye kujieleza kuhusu alichotaka kutoka kwangu" Alisema.
Malkia huyo pia aliweka wazi kwamba hajawahi kuishi katika nyumba moja na mwanamume yeyote maishani mwake.
Alisema kwamba amekuwa akiishi pekee yake na hata wafanyikazi wake huenda pale kwake ifikapo wikendi pekee.