Otile Brown atoa taarifa nzuri kuhusu afya yake baada ya upasuaji

Wiki iliyopita Brown alitoa taarifa ya kutia wasiwasi kuhusu afya yake.

Muhtasari

•Mwanamuziki huyo ametoa taarifa mpya kuhusu afya yake huku akifichua kuwa afya yake imeendelea kuimarika.

•Nabbi ambaye alitengana na Otile Brown wiki chache zilizopita amemtakia baraka na ulinzi wa Mola katika siku zote za maisha yake.

Image: INSTAGRAM// OTILE BROWN

Mapema mwezi huu mwanamuziki mashuhuri Jacob Obunga almaarufu kama Otile Brown alifanyiwa upasuaji katika hospitali moja jijini Nairobi.

Brown alitangazia mashabiki wake kuhusu upasuaji huo kupitia ukurasa wake wa Instagram ambapo alipakia video iliyoonyesha akiwa amelazwa kitandani cha hospitali na akaeleza kuwa shughuli hiyo iliendelea vizuri.

Siku chache baadae hata hivyo, Brown ambaye anashabikiwa sana hasa katika kanda ya Afrika Mashariki alitoa taarifa ya kutia wasiwasi kuhusu afya yake.

"Nina maumivu makali sana..ombeeni Obizee" Brown alitangaza kupitia ukurasa wake wa Instagram.

Siku ya Jumatano mwanamuziki huyo alitoa taarifa mpya kuhusu afya yake huku akifichua kuwa afya yake imeendelea kuimarika.

Otile aliendelea kutangaza kuwa atakuwa anasafiri kuelekea Bahrain ambako atatumbuiza Jumatano wiki ijayo.

"Obizee anaendelea vyema.. Bahrain, naja wiki ijayo, Jumatano tarehe 23" Otile alitangaza.

Mamia ya mashabiki wameendelea kumtakia msanii huyo afueni ya haraka tangu alipotangaza kuhusu upasuaji.

Mpenzi wake wa zamani Nabayet almaarufu kama Nabbi ni mmoja wa waliomkumbuka katika kipindi hiki kigumu. 

Nabbi ambaye alitengana na Otile Brown wiki chache zilizopita amemtakia baraka na ulinzi wa Mola katika siku zote za maisha yake.