Mchekeshaji Akuku Danger azungumzia maendeleo ya afya yake baada ya kulazwa mara mbili

Akuku Danger ametaja kipindi ambacho alikuwa amelazwa hospitalini kama "Yote ilikuwa giza."

Muhtasari

•Akishirikisha mashabiki wake katika kipindi cha maswali na majibu kwenye mtandao wa Instagram, Akuku Danger alifichua kuwa sasa yuko karibu kupona kabisa.

•Hata hivyo amefichua kuwa bado hawajafanikiwa kulipa bili yote ya hospitali na kueleza kuwa kuna salio la shilingi Sh1.3M.

Akuku azungumzia maendeleo ya afya yake
Akuku azungumzia maendeleo ya afya yake
Image: INSTAGRAM

Mchekeshaji wa Churchill Show Akuku Danger amesema kuwa anaendelea kupata afueni baada ya kulazwa hospitalini mara mbili mapema mwaka huu.

Akishirikisha mashabiki wake katika kipindi cha maswali na majibu kwenye mtandao wa Instagram, Akuku Danger alifichua kuwa sasa yuko karibu kupona kabisa.

Mchekeshaji huyo hata hivyo alieleza kuwa tangu aruhusiwe kutoka hospitali hajakuwa akifanya kazi nyingi kwani amekuwa akipumzika nyumbani tu katika juhudi za kuimarisha afya yake.

"Niko karibu kupona.. nimekuwa sawa, bado napumzika nyumbani.. naponapona," Akuku Danger alijibu mashabiki waliotaka kufahamu kuhusu afya yake kwa sasa.

Mchekeshaji huyo alieleza hamu yake kubwa ya kurejea kwenye kazi yake ya uchekeshaji huku akihakikishia mashabiki kuwa atarejea hivi karibuni.

Hata hivyo amefichua kuwa bado hawajafanikiwa kulipa bili yote ya hospitali na kueleza kuwa kuna salio la shilingi Sh1.3M.

"Bili bado haijakamilika kulipwa. Shilingi milioni 1.3 bado zimesalia. Paybill bado inaendelea 891300," Alisema.

Mwaka wa 2022 haukuanza vyema kwa mchekeshaji Akuku Danger kwani ulimpata hospitalini akiwa amelazwa kufuatia matatizo ya kupumua.

Afya  yake ilidhoofika kiasi cha kwamba alilazwa katika chumba cha mahututi. Takriban wiki moja baada ya kuruhusiwa kutoka hospitalini  mara ya kwanza, mchekeshaji huyo alilazwa tena baada ya kushambuliwa na matatizo mengine.

Akuku Danger ametaja kipindi ambacho alikuwa amelazwa hospitalini kama "Yote ilikuwa giza."