Mapema wiki hii dunia iliadhimisha siku ya wanawake. Kwa kawaida, Machi 8 ndio tarehe maalum iliyotengwa kuwasherehekea wanawake wote duniani.
Walimwengu walitumia njia tofauti kusherehekea wanawake muhimu maishani mwao zikiwemo kuwapa maua na zawadi, kuwaandikia jumbe tamu, kuwapeleka dates na zinginezo.
Wengi walisherehekea mama zao, wake wao, dada, mabinti, wafanyi kazi wenza kati ya wanawake wengine muhimu katika maisha yao.
Nyota wa Bongo Diamond Platnumz hakusalia nyuma huku akitumia fursa hiyo kuonyesha dunia wanawake anaothamini sana maishani.
Mwanamuziki huyo alitumia ukurasa wake wa Instagram kusherehekea mamake Sanura Kassim almaarufu Mama Dangote, dada zake Esma Platnumz na Queen Darleen, binti yake Tiffah Dangote na msanii wake Zuchu.
Diamond alipakia picha za watano hao na kuziambatanisha na jumbe tamu na emoji zinazoashiria upendo.
Licha ya kuwa na baby mamas watatu wanaojulikana; Hamisa Mobetto, Zari Hassan na Tanasha Donna, kigogo huyo wa muziki hakusherehekea yeyote kati yao.
Mwezi uliopita, baba huyo wa watoto wanne wanaojulikana alikiri kuwa kwenye mahusiano na ilitarajiwa huenda pia angemsherehekea mpenzi huyo wake asiyetambulishwa ila hilo halikutokea.
Kulikuwa na uvumi kuwa anachumbiana na msanii wake Zuchu na ingawa wote wawili walipuuzilia mbali madai hayo, hatua yake kumsherehekea huenda ikatilia shaka uhusiano wao.
Diamond anajulikana kuwa kipenzi cha wanawake na hata mwenyewe amewahi kukiri kuwa 'player'. Anaaminika kuwahi chumbia zaidi ya wanawake kumi kutoka mataifa mbalimbali.