Sallam SK ambaye ni meneja wa kazi za muziki za msanii nambari moja wa siku zote Diamond Platnumz na lebo ya WCB Wasafi kwa ujumla amewaomba mashabiki na wafuasi wa lebo hiyo kumruhusu kustaafu kutoka kazi hiyo.
Sallam ambaye pia wengi wanamfahamu kwa jina lingine kama Mendez, kwa kile kilichoonekana kama ni kuwatania wafuasi na mashabiki wa Wasafi, alisema kwamba anaomba kustaafu baada ya kupewa ngoma 40 za EP ya FOA na akazichagua kumi tu na kuziacha pembeni ngoma 30.
“Naomba nitangaze kustaafu kama mtaniruhusu, nilipewa nyimbo 40 nimechagua 10 bado 30,” alisema Sallam SK.
EP ya Diamond ya First Of All (FOA) iliachiwa rasmi siku wa kuamkia Ijumaa wiki jana ikiwa na nyimbo 10 huku wasanii watano wakishiriki kwenye EP hiyo ambao ni Zuchu, Mbosso, Adekunle Gold, Jaywillz, Focalistic, Costa Titch na Pabi Cooper.
Hadi kufikia sasa, EP hiyo inazidi kutesa kwenye anga na mitabendi zote katika zaidi ya mataifa 28 kote barani Afrika.
Katika kutaja mafanikio ya msanii Diamond kimuziki, bila shaka hadithi yote haitamalizika bila jina la Mendez kutamkika tena kwa herufi kubwa za dhahabu kutokana na ueledi wake mkubwa katika kufanikisha msanii huyo anakwea kwenye kilele cha juu kabisa kimuziki si tu Afrika mashariki bali bara la Afrika kwa ujumla.
Mwezi jana Mendez alisutwa vikali na wapenzi wa muziki kwa kuruhusu Diamond kuweka picha ya bendera ya Confederate kwenye video ya single yake mpya ya Gidi, jambo ambalo lilizua maoni kinzani kutokana na kwamba bendera hiyo ina historia mbaya ya ubaguzi wa rangi kwa Wamarekani Weusi.