"Siwezi kubali umaskini unaopiga msanii akizeeka" Guardian Angel azungumzia mipango yake ya baadaye

Muhtasari

•Mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka 33 amesema kwa kuwa bado ana nguvu, anatumia fursa hiyo kujiandaa kwa maisha ya uzeeni.

•Amedokeza kwamba anapanga kustaafu baada ya miaka mitano ili aweze kuponda mali yake polepole pamoja na mkewe.

Esther Musila na mumewe Guardian Angel
Esther Musila na mumewe Guardian Angel
Image: INSTAGRAM//GUARDIAN ANGEL

Mwimbaji wa nyimbo za injili Peter Omwaka almaarufu Guardian Angel amefichua kwamba anaendelea kujenga makao ya kudumu kama njia ya kujipanga  kwa maisha ya usoni na mkewe Esther Musila.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Guardian Angel alionyesha ujenzi wa nyumba ya nguruwe unaoendelea  katika kiwanja chake.

Mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka 33 amesema kwa kuwa bado ana nguvu, anatumia fursa hiyo kujiandaa kwa maisha ya uzeeni.

"Kazi juu ya kazi... Nyumba mpya ya nguruwe wetu. Siwezi kubali ile umaskini hupiga msanii akizeeka kwa nchi hii. Napiga sana kama nguvu iko," Guardian Angel alisema.

Amedokeza kwamba anapanga kustaafu baada ya miaka mitano ili aweze kuponda mali yake polepole pamoja na mkewe.

Guardian Angel na Bi Musila walifunga pingu za maisha mwezi Januari mwaka huu katika harusi ndogo iliyohudhuriwa na wanafamilia na baadhi ya marafiki wa karibu.

Wawili hao walikutana mwaka wa 2020 na penzi lao likaendelea kunoga hadi kufikia hatua ya ndoa. Hata hivyo wamekabiliana na pingamizi kubwa mitandaoni haswa kutokana na pengo kubwa katika umri wao.

Bi Musila ana umri wa miaka 52 na ana watoto watatu wakubwa ambao alipata katika ndoa yake ya hapo awali.

Esther Musila na mumewe Guardian Angel
Esther Musila na mumewe Guardian Angel
Image: INSTAGRAM//GUARDIAN ANGEL