Bi Sanura Kassim almaarufu Mama Dangote amedokeza kwamba mwanawe Diamond Platnumz hatimaye amepata mchumba mpya.
Mama Dangote ameonekana kupendezwa sana na mpenzi mpya wa nyota huyo wa Bongo hadi kushindwa kuzuilia furaha yake.
"Nashindwa kuelezea furaha yangu mwanangu, Naseeb Diamond Platnumz🦁, hapa sasa umepata mwenza," Mama Dangote alisema kupitia ukurasa wake wa Instagram.
Kwa vile ameridhishwa na mkaza mwanawe mtarajiwa, Mama Dangote amemshauri mwanawe atulie sasa na afunge pingu za maisha naye.
"Utulie babangu uoe.." Alisema.
Mamake Diamond hata hivyo hakufichua ni mwanadada yupi huyo kateka moyo wa mwanawe kiasi cha kwamba harusi yanukia.
Haya yanajiri wiki kadhaa baada ya Diamond Platnumz kukiri kwamba yupo kwenye mahusiano.
Mwezi Februari, katika msimu wa wapendanao, Diamond alikiri kwamba anayafurahia sana mahusiano yake mapya
"Niko kwenye mahusiano. Nina furaha. Nafurahia, mahusiano yangu yananipa raha na amani. Huba limetaradadi, mahaba ndi ndi ndi" Diamond alisema.
Diamond aliweka wazi kwamba anampenda sana malkia anayechumbia kwa sasa na kudhihirisha kuwa anayathamini mahusiano yao. Hata hivyo hakufichua chochote kuhusu mpenzi wake mpya.