"Hatujawahi kukutana!" Diana Marua azungumzia ugomvi wake na mke wa Mr Seed, Nimo Gachuiri

Walikosana mwaka wa 2019

Muhtasari

•Mke huyo wa Bahati alifichua kuwa yeye na Nimo hawajahi kupata nafasi ya kukutana moja kwa moja tangu walipotofautiana.

•Diana alisema uhusiano wao kwa sasa ni mzuri na hata wamewahi kuzungumza kwa simu katika kipindi hicho.

Diana Marua na Nimo Gachuiri
Diana Marua na Nimo Gachuiri
Image: HISANI

Mwanavlogu mashuhuri Diana Marua ameweka wazi kwamba kwa sasa hakuna uhasama wowote kati yake na mwanamuziki Nimo Gachuiri.

Akizungumza na wanahabari Jumamosi, Diana hata hivyo alikiri kuwa hapo awali kuliwahi kutokea tofauti kati yake na mke huyo wa Mr Seed.

"Watu hufanya makosa katika miaka yao ya awali. Kadri siku zinavyosonga unakuja kugundua  kuwa labda sikuwa mzima kutosha kushughulikia suala fulani kwa njia nzuri. Unakua kutoka hapo. Wakati mwingine sio lazima ujitokeze kuomba msamaha. Maisha hutupatia mafunzo kwa njia tofauti," Diana alisema.

Mke huyo wa Bahati alifichua kuwa yeye na Nimo hawajahi kupata nafasi ya kukutana moja kwa moja tangu walipotofautiana.

Licha ya kuwa hawajakuwa wakikutana baada ya kutofautiana, Diana alisema uhusiano wao kwa sasa ni mzuri na hata wamewahi kuzungumza kwa simu katika kipindi hicho.

"Sina beef na yeye. Hata kuna wakati nilikuwa napitia mambo fulani na alinipigia simu. Mimi sina shida yoyote naye. Hakuna haja eti tukae chini tusameheane. Hakuna shida. Tuko sawa,"Diana alisema.

Wawili hao walikutana  kwa mara ya kwanza katika tamasha iliyofanyika Jumamosi baada ya kipindi cha takriban miaka mitatu.

Walikosana mwaka wa 2019 kufuatia madai kuwa Diana aliita polisi wamkamate Nimo, ambaye kwa wakati huo alikuwa mjamzito, kwa sababu alitaka kufanya biashara wakati wa hafla iliyoandaliwa na Bahati.