Mwanavlogu Diana Marua na Yvette Obura wamefichua kuwa iliwachukua muda mrefu kuweza kujenga uhusiano wao mzuri.
Wawili hao ambao wote wana watoto na mwanamuziki Bahati wamekiri kuwa walitofautiana na kuvurutana miaka ya hapo awali kabla ya kufikia hatua ya kutamatisha ugomvi wao na kushirikiana.
Katika mazungumzo kwenye chaneli yake ya Youtube, Diana alifichua kuwa ugomvi wake na Yvette ulianza baada yake kupakia picha aliyopigwa pamoja na binti ya Yvette.
"Mimi nilipost picha tu. Wanamitandao walianza kunishambulia wakisema ningemuuliza mamake kwanza. Kulikuwa na mambo mengi. Nilisema uharibifu umeganyika tayari na hakuna kitu ambacho ningeweza kufanya. Nilidhani kitu cha maana kufanya ni kufanya ni kufuta picha lakini Baha alisema nisifute. Hapo ndipo beef ilianza rasmi. Nadhani mimi ndio nilichokoza nyuki," Diana alisema.
Diana ni mke wa sasa wa Bahati ilhali Yvette ni mpenzi wa zamani na baby mama wa mwanamuziki huyo.
Baada ya wawili hao kutofautiana kuhusu suala la picha kulizuka mvutano kati yao kwa muda kabla ya kukubaliana kusuluhisha mizozo yao.
Yvette ambaye pia anatambulika kama Mama Mueni alifichua alimfikia Diana kupitia mtandao wa Instagram akiomba msamaha kwa yaliyotokea kati yao.
"Nilichukua simu yangu nikakuandikia (Bahati), 'Umekuwa mama mzuri kwa Mueni kutokana na yale ambayo huwa ananiambia. Pole kama nimewahi kukosea ama kufanya maisha yako yawe mazuri. Nisamehe na ningetaka tuwe mahali pazuri'. Kusema kweli sikudhani ungejibu," Yvette alimwambia Diana.
Wawili hao walifichua kuwa walilazimika kushirikiana katika malezi ya Mueni baada ya Bahati kuwaagiza wawe wanawasiliana.
Diana aliweka wazi kuwa Yvette hakuwahi kumkosea heshima licha ya kuwa kulikuwa na ugomvi kati yao.