Fahamu mzozo kati ya Diamond na dini uliopelekea video ya 'Mtasubiri' kupigwa marufuku

Muhtasari

• Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) iliipiga marufuku video kufuatia malalamishi ya baadhi ya waumini wa madhebehu ya dini nchini humo.

•Diamond ametakiwa kurekebisha sehemu iliyozua utata ili video hiyo kuruhusiwa kutumika tena.

Image: YOUTUBE// DIAMOND PLATNUMZ

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imeviandikia vyombo vyote vya habari nchini humu ikiviagiza kutocheza video ya wimbo 'Mtasubiri sana' wake Diamond Platnumz akishirikiana na Zuchu.

Hii ni baada ya Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) kuipiga marufuku video kufuatia malalamishi ya baadhi ya waumini wa madhebehu ya dini nchini humo.

Kikundi cha waumini kiliwasilisha ombi la kufutwa kwa video hiyo wakidai kuwa kuna kipande ambacho kinaashiria dharau kwa dini fulani.

"Msanii tajwa (Diamond Platnumz) ametoa video ya wimbo unaofahamika kama 'Mtasubiri Sana' na katika video hiyo kuna kipande kimeonyesha wahusika wapo kanisani wanaimba kwaya lakini baadae wakaacha na kuelekea kwingine. Kipande hicho cha video kimeleta ukakasi miongoni mwa waumini wa madhebehu ya dini na kuleta hisia kwamba ni dharau ya dini/madhebehu fulani," Taarifa iliyopigwa saini na Mkurugenzi Mtendaji wa TCRA Dkt Jabiri K. Bakari ilisoma.

Aidha, TCRA imeviagiza vyombo vya utangazaji na mitandao ya kijamii nchini Tanzania kutosambaza video ya wimbo huo hadi marekebisho yatakapofanya.

"Baraza la Sanaa kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania wana wajibu wa kusimamia maadili ya Sanaa na maudhui ya kazi za Sanaa zinazosikilizwa au kutazamwa na Umma wa Tanzania," Taarifa ilisoma.

Video ya wimbo 'Mtasubiri sana' iliachiwakwenye mtandao wa Youtube mnamo Machi 29, 2022 na kufikia hatua ya kupigwa marufuku ilikuwa imepata views zaidi ya milioni kumi.

Diamond ametakiwa kurekebisha sehemu iliyozua utata ili video hiyo kuruhusiwa kutumika tena.