"Nilisikitika sana!" YY azungumza baada ya Alvin Chivondo kupatikana akiiba tena Naivas

Muhtasari

•Alhamisi wiki iliyopita Chivondo alitiwa mbaroni tena baada ya kupatikana akiiba katika duka la Naivas jijini Nairobi.

•YY amesema kuwa wakati alipojitolea kumsaidia Alvin alidhani angekubali kubadilisha mienendo yake ya uhalifu.

Image: INSTAGRAM// YY COMEDIAN

Mchekeshaji Oliver Otieno almaarufu YY amesema alivunjwa moyo sana baada ya kuona Alvin Chivondo akirudia kosa la wizi ambalo alikuwa ameshtakiwa nalo.

Akiwa kwenye mahojiano na Eve Mungai, YY alisema kuwa wakati alipojitolea kumsaidia Alvin alidhani angekubali kubadilisha mienendo yake ya uhalifu.

Mchekeshaji huyo amesema kuwa Alvin sasa anafaa kukabiliana na matokeo ya matendo yake ya wizi.

"Kila kitu kilifanyaka kulingana na sheria. Wakati huu wacha akabiliane na sheria. Ni kama anahisi kwa kuwa hakukuwa na matokeo ndio maana aliona arudie kosa hilo. Hakuhisi uchungu wowote, alikaa gerezani siku moja tu. Wacha akae muda mrefu itakuwa funzo kubwa kwake," YY alisema.

Alhamisi wiki iliyopita Chivondo alitiwa mbaroni tena baada ya kupatikana akiiba katika duka la Naivas jijini Nairobi.

Chivondo alipatikana akiiba unga wa mahindi takriban mwezi mmoja tu baada ya aliyekuwa gavana wa Nairobi Mike Sonko kumlipia faini ya Sh100,000 ambayo aliagizwa kulipa na mahakama kwa  kosa la kuiba mchele kilo 5, mafuta ya kupikia lita 5 na sukari kilo 2 katika duka hilo hilo la Naivas.

YY alikuwa amejitolea kumsaidia Chivondo kulipa faini hiyo ili aepuke kifungo cha mwaka mmoja gerezani kabla ya Sonko kupiga hatua hiyo mbele yake. Mchekeshaji huyo hata hivyo alitumia fedha ambazo alichangisha kumsaidia Chivondo katika mambo mengine ya kinyumbani k.v kununua bidhaa, kulipa kodi na mengineo.

YY anasema kuwa huenda jamaa huyo anafanya kazi na genge fulani ambalo linahusika na bidhaa zilizoibiwa.

"Nadhani hiyo kitu anafanya ni ya ucartel. Juu kama uko na shopping, uko na chakula na uko na kazi kisha unaenda kuiba inamaanisha kuna mahali wanapeleka hizi vitu. Kuna nia tofauti. Sijui mbona alichagua duka hilohilo. Hiyo ni tabia yake," Alisema.

Mchekeshaji huyo pia alifichua kuwa baada ya kumsaidia Chivondo baadhi ya wanafamilia wake walimdokezea kuwa yeye ni mhalifu wa kawaida.

YY pia alifichua kuwa  kabla ya kukamatwa tena Chivondo alikuwa  na mazoea ya kumuomba pesa na vitu vingine mara kwa mara.

Pia alisema amekuwa akijaribu kumpigia mkewe simu lakini bado hajaweza kufua dafu.