"Sijui kilichotokea, nilijipata chini" Omosh azungumzia kipindi cha maombi na Pastor Kanyari

Muhtasari

•Omosh amedai kuwa alijipata tu ameanguka na hakufahamu ni nini kilichotokea wakati wa maombi ambacho kilimsukuma chini.

•Pia amekana madai kuwa Kanyari alikuwa anatoa pepo kutoka kwake huku akiweka wazi kuwa mhubiri huyo alikuwa anaombea taaluma yake ya usanii.

Omosh akiombewa na Pastor Kanyari
Omosh akiombewa na Pastor Kanyari
Image: SCREENGRAB

Muigizaji wa Tahidi High Joseph Kinuthia almaarufu Omosh amepuuzilia mbali madai kuwa  kuanguka kwake wakati alipokuwa akiombewa na mhubiri Victor Kanyari ilikuwa maigizo tu.

Omosh amedai kuwa alijipata tu ameanguka na hakufahamu ni nini kilichotokea wakati wa maombi ambacho kilimsukuma chini.

Muigizaji huyo amesema kuwa yeye ni muumini wa kweli na kusisitiza kuwa kamwe hawezi kufanya maigizo kanisani.

"Siwezi kusimulia kilichotokea. Kitambo nilidhani watu huwa wanajifanya wakianguka. Watu wanaichukulia kama maigizo. Hata hivyo kuna nguvu katika maombi. Sijui kilichotokea lakini nilijipata chini.Nilijipata naenda na nikafika. Yule jamaa alikuwa ananichapa tu. Wakati alikuwa ananiombea nami nilikuwa naomba. Nilijipata tu nikienda. Mimi ni Mkristo na siwezi kucheza na madhabahu au neno la Mungu. Mimi naamini kulikuwa na nguvu pale," Omosh alisema.

Omosh amesisitiza kuwa ana heshima kubwa kwa Mungu na kuwaomba watu kusita kuhukumu tukio hilo.

Pia amekana madai kuwa Kanyari alikuwa anatoa pepo kutoka kwake huku akiweka wazi kuwa mhubiri huyo alikuwa anaombea taaluma yake ya usanii.

"Watu wanasema nilienda kutolewa mapepo. Mimi sina pepo. Alikuwa anaombea taaluma yangu ikue. Maoombi yalikuwa mazuri. Hakukuwa na stori na pepo," Alisema.

"Vile watu watasema waseme lakini mimi naamini niliguswa na Mungu,"

Mapema wiki hii video ya muigizaji huyo akianguka wakati akiombewa na mhubiri Victor Kanyari ilisambaa mitandaoni.

Wanamitandao walitoa hisia mbalimbali kutokana na tukio hilo baadhi wakipongeza hatua yake kuenda kuombewa huku wengine wakidai kuwa ni maigizo.

Mwimbaji wa nyimbio za injili Ringtone Apoko ni miongoni mwa wengi ambao walidai kuwa Omosh alikuwa anatolewa mapepo na mhubiri huyo.