"Utakumbukwa milele na daima" Omosh amuomboleza baba yake

Muhtasari

•Omosh alitangaza kuhusu kifo cha mzazi huyo wake Jumapili na kumtaja marehemu kama mtu mzuri ambaye atakumbukwa milele.

•Marehemu pia ni baba ya muigizaji mkongwe Naomi Kamau ambaye aliigiza kama mama ya Tina na Mike katika kipindi cha Mother-in-Law.

Image: INSTAGRAM// OMOSH KIZANGILA

Muigizaji Joseph Kinuthia almaarufu Omosh kutokana na kipindi cha Tahidi High yupo katika hali ya kuomboleza baada ya kufiwa na babake mzazi.

Omosh alitangaza kuhusu kifo cha mzazi huyo wake Jumapili na kumtaja marehemu kama mtu mzuri ambaye atakumbukwa milele.

Huku akimtakia mapumziko ya amani Omosh, alisema babake atakumbukwa zaidi kutokana na nyakati nzuri ambazo alishiriki nao.

"Utakumbukwa milele na milele. Matukio mazuri uliyoshiriki nasi daima yatazungumza juu ya mtu bora ambaye ulikuwa. Pumzika kwa amani Baba," Omosh alisema kupitia ukurasa wake wa Instagram.

Mchekeshaji huyo aliambatanisha ujumbe wake na picha inayoonyesha akiwa amemshika mzazi huyo wake kwenye bega.

Marehemu pia ni baba ya muigizaji mkongwe Naomi Kamau ambaye aliigiza kama mama ya Tina na Mike katika kipindi cha Mother-in-Law.

Haya yanajiri katika kipindi ambapo Omosh ameanza kufufua taaluma yake ya usanii baada ya kuwa amezama kwenye uraibu wa pombe kwa muda mrefu.

Katika mahojiano ya hapo awali muigizaji huyo alifichua kuwa alikuwa ameathirika na uraibu wa pombe kwa takriban miongo miwili.

"Nilikuwa mraibu kwa takriban miaka 20. Wakati huo singeweza kula ama kunywa chai asubuhi kama sijachomwa. Asubuhi nikiamka ningetoa sababu yoyote ili nitoke kwa nyumba ndio niende nikakunnywe," Omosh alisema akiwa kwenye mahojiano na Grace Makena.

Alisema alikaa miaka minne bila kuonja mvinyo baada ya kupelekwa rehab. Hata hivyo janga la Corona lilipokumba dunia alijipata kwenye majaribu na kuanza kulewa tena na hapo masaibu zaidi yakaanza.

Siku kadhaa zilizopita muigizaji huyo alihudhuria ibada katika kanisa la mhubiri mashuhuri Victor Kanyari ambaye aliombea taaluma yake na kumkabidhi zawadi kemkem.