Muigizaji Malik Lemmy almaarufu Govi kutokana na kipindi Machachari amesisitiza kuwa anapendelea kuchumbiana na wanawake waliomzidi umri.
Akiwa kwenye mahojiano na Mpasho, Govi alikiri kuwa wanawake wengi ambao amewahi kuchumbiana nao hapo awali ni wakubwa zaidi yake kwa angalau siku moja au zaidi.
"Niko wazi kuchumbiana na msichana wa aina yoyote lakini kwa muda mrefu upendeleo wangu umekuwa wanawake wakubwa," Govi alisema.
Hata hivyo aliweka wazi kuwa mwanadada mkubwa zaidi ambaye aliwahi kuwa kwenye mahusiano naye alimzidi umri kwa miaka minne.
"Nadhani hapo ndo kikomo changu. Miaka minne kuenda chini ni sawa. Miaka minne kuenda juu siwezi," Alisema.
Govi ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 21 amekuwa katika tasnia ya uigizaji kwa takriban miaka 17.
Muigizaji huyo wa zamani wa Machachari alibainisha kuwa kukua karibu na watu wakubwa na kuwa hadharani kwa muda mrefu kuliathiri mapendeleo yake kwa wanawake.
"Kukaa na wakubwa ilifanya nikaona siwezi kukaa na watoto. Mtu huwa na hamu ya kuwa kama yule mtu ambaye umekua ukimuona kwenye runinga. Nimefanya kazi kwa miaka 17," Alisema.
Govi vilevile alieleza kuwa hali ya kukua karibu na watu wakubwa ilimfanya atende na kufikiri tofauti na watoto wengine.
Muigizaji huyo pia alifunguka kuhusu upendo wake mkubwa kwa wanyama kipenzi (pets). Alifichua kuwa amewahi kufuga zaidi ya paka 200 na mbwa 6.
"Saa hii niko paka watano na mbwa watatu," Alisema.
Alisema kwamba huwa anawafuga wanyama hao ndani ya nyumba yake.