Mwanamuziki Kelvin Kioko almaarufu Bahati amesema madai kuwa mke wake Diana Marua ni mjamzito ni makisio ya watu tu.
Wanandoa hao mashuhuri walipokuwa wakihutubia waandishi wa habari katika hafla ambayo waliandaa kwa ajili ya kukutana na wanafamilia na marafiki wao waliweka wazi kuwa hawana uhakika ikiwa wanatarajia mtoto wa tatu pamoja hivi karibuni.
Bahati ambaye tayari ni baba ya watoto watatu hata hivyo aliahidi kuwa watapiga hatua ya kutembelea hospitali ili kubaini ikiwa kwa kweli Diana ni mjamzito.
"Kwani kuna watu wanakuwanga bedroom yetu. Ni maoni tu. Kusema kweli wamekisia sana, tutaenda hospitali tupime. Haiwezi kuwa watu wanakisia na sijui," Bahati alisema.
Diana Marua kwa upande wake alisita kuthibitisha ama kukana ikiwa kuna kiumbe anachobeba tumboni kwa sasa.
"Sijui!" Diana alisema alipoagizwa na mumewe kujibu ikiwa ana ujauzito.
Wanandoa hao walilazimika kuzungumzia suala hilo kufuatia uvumi mwingi uliosambazwa kwenye mitandao ya kijamii kuwa wanatarajia mtoto wao wa tatu.
Katika siku za hivi majuzi wanamitandao wamekuwa wakiangazia tumbo la Diana linalochomoza mara nyingi anapopakia picha zake kwenye mitandao ya kijamii wakidai kuwa huenda ni mjamzito.
Diana na Bahati tayari wana watoto wawili pamoja. Wanandoa hao walibarikiwa na mtoto wa kwanza pamoja, Heaven Bahati, mwezi Februari 2018.
Mnamo Agosti 14, 2019 wanandoa hao walikaribisha mtoto wao wawili pamoja, Majesty Bahati.
Isitoshe, wawili hao pia wameadopt mvulana mmoja anayetambulika kama Morgan Bahati. Bahati alimchukua Morgan kama mtoto wake takriban miaka nane iliyopita.
Bahati pia ana mtoto mwingine wa kike, Mueni Bahati, ambaye alipata na aliyekuwa mpenzi wake kabla ya Diana, Yvette Obura.