Msanii Bahati Kioko ameonekana kujutia mkondo alioufuata wa kujitosa kwenye siasa baada ya kupakia picha kwenye Instagram yake na kusema kwamba amejionea vitu vingi sana katika siasa na ambavyo pengine kama msanii angeishia kuvisikia tu kwenye majarida na vyombo vya habari.
Bahati pia amemhurumia mkewe, Diana Marua na kusema kwamba wanawake wengine wakati wanawapetipeti wanaume wao yeye yuko tu anahaha juu chini kuhakikisha kwamba mumewe hasababishiwi kulia tena.
“Wakati Wanandoa Wengine Wakifurahia Ndoa zao Mke wangu yuko Busy Kuhakikisha kwamba Silii tena. Aki Vitu Nimepitia Kwa Siasa Wewe,” aliandika Bahati.
Msanii huyo ameachia maneno haya siku moja tu baada ya video kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii ikimuonesha anafurushwa kutoka mkutano wa kisiasa ulioandaliwa Mathare na viongozi kutoka muungano wa Azimio-One Kenya wa kaunti ya Nairobi.
Bahati baadae alijitokeza na kupuuzilia mbali video hiyo huku akiibua madai upya kwamba katibu mkuu wa chama cha ODM, Edwin Sifuna ndiye aliyeahirisha mkutano huo kinyume na matakwa ya hadhira pindi alipomuona Bahati anaingia akiongozana na wafuasi wake.
Maneno hayo kwamba mkewe anahangaika kuhakikisha asilie yalimkuta Diana Marua kwa kicheko kikubwa ambapo alitoa maoni yake na kusema kwamba hilo limempata barabara japo awali alikuwa amempa motisha kweli mumewe kutoacha azma yake ya kuwania ubunge Mathare.
Ikumbukwe Bahati aliposemekana kuzuiwa na chama cha Jubilee dhidi ya kuwania ubunge licha ya kushinda tikiti ya chama hicho katika uchaguzi wa mchujo mwezi Aprili, msanii huyo alitokwa na machozi mbele ya wanahabari, akidai kuhujumiwa lakini baadae alipewa tikiti na kukubaliwa kuwania.