Jinsi watu mashuhuri walivyoomba msamaha hadharani baada ya kuwakosea wapenzi wao

Kunao wasanii ambao wamejijaza ujasiri, wakakiri makosa yao na kuomba radhi hadharani kwa wapenzi wao baada ya kuwakosea

Muhtasari

•Jumamosi Jimal aliandika ujumbe mrefu wa kuomba msamaha kwa mkewe na kukiri kuwa alimkosea kwa kuingiza drama nyingi kwenye ndoa yao.

Jimal Marlow Rohosafi, Harmonize, Nyota Ndogo, Samidoh
Image: INSTAGRAM

Moja ya stori ambazo zilivuma sana mtandaoni wikendi ni ile ya mfanyibiashara Jimal Marlow Rohosafi kumuomba msamaha mkewe Amira kufuatia drama nyingi  alizoleta kwenye ndoa yao mwaka jana hadi kufikia kuivunja.

Jumamosi Jimal aliandika ujumbe mrefu wa kuomba msamaha kwa mkewe na kukiri kuwa alimkosea sana mama huyo wa watoto wake wawili kwa kuingiza drama nyingi kwenye ndoa yao ya miaka mingi.

"Naomba radhi kwa kukukosea heshima, kukuaibisha, kwa kukuumiza, kwa maumivu yote na kwa huzuni niliyokuletea. đź’”Samahani kwa nyakati zote ambazo sijawa mwanaume niliyeahidi kuwa," Jamal alimuandikia mkewe.

Mwenyekiti huyo wa Muungano wa Wamiliki Matatu jijini Nairobi alikiri kwamba alikosa kutimiza  wajibu wake wa kumlinda mkewe na kudai kwamba hajakuwa sawa tangu alipokosana naye.

Katika ile iliyoonekana kama jibu kwa mumewe, Amira alitangaza kuwa angehutubia watu kuhusiana na suala hilo baada ya kurejea nchini kutoka Tanzania.

Jimal sio mtu mashuhuri wa kwanza kuomba msamaha hadharani katika siku za hivi majuzi baada ya kumkosea mwenzie.

Hawa hapa baadhi ya watu mashuri ambao wamechukua hatua kama ya Jimal:

(i) Harmonize kwa Kajala

Image: instagram//harmonize

 Miezi michache ambayo imepita Harmonize alianza harakati za kuomba msamaha kutoka kwa muigizaji Frida Kajala Masanja.

Wawili hao walikosana mapema mwaka jana kufuatia madai kuwa Kajala aligundua Harmonize alikuwa anamtongoza bintiye Paula Kajala.

Licha ya uzito wa tuhuma hizo Kajala hatimaye aliridhia msamaha wa Harmonize na kwa sasa tayari wamerudiana na kuvishana pete za uchumba.

ii) Profesa Hamo kwa Jemutai

Mwaka jana mchekeshaji Profesa Hamo alilazimika kuomba msamaha kwa mzazi mwenzake Jemutai baada ya kudaiwa kutekeleza watoto wao wawili.

Wawili hao waliwasha moto mkubwa kwenye mitandao ya kijamii huku wakishiriki katika vuta nikuvute kwa muda.

Hamo  hata hivyo hatimaye aliomba msamaha na kuahidi kuwa baba mzuri baada ya vipimo vya DNA kuthibitisha kuwa watoto wote wawili ni wake.

Image: FACEBOOK// JEMUTAI

iii) Samidoh kwa Edday Ndiritu

Mapema mwaka jana staa wa Mugithi Samuel Muchoki almaarufu Samidoh alizama mitandaoni kumuomba msamaha mkewe Edday Ndiritu baada ya kusakata ngoma nje ya ndoa.

Samidoh alijihusisha kwenye mahusiano ya kando na wakili Karen Nyamu na hata kupata mtoto pamoja.

Mwanamuziki huyo alikiri makosa yake na kuwaomba msamaha mkewe na mashabiki. Pia aliweka wazi kuwa hakumtema mkewe.

iv) Sarah Kabu kwa Simon Kabu

Mapema mwaka huu mjasiriamali Sarah Kabu alichukua hatua ya kumuomba msamaha mumewe Simon Kabu baada ya kuanika ya mambo ya ndani ya ndoa yao.

Sarah alikuwa amefichua jinsi mumewe alichukua watoto wao na kuwapeleka likizo  pamoja na binti yake mkubwa.

Baadae katika mahojiano ya YouTube alikiri kumkosea mumewe na kuomba msamaha kwake. Hali ya amani hatimaye ilirejea kwa ndoa yao na hata wanatarajia mtoto mwingine pamoja hivi karibuni.

Sarah Kabu na Simon Kabu
Sarah Kabu na Simon Kabu
Image: HISANI

v) Abel Mutua kwa Judy Nyawira

Hivi majuzi muigizaji Abel Mutua alilazimika kuomba msamaha kufuatia shinikizo kubwa la wanamitandao waliodai alimuacha mkewe katika hali ya upweke kwenye tamasha ya Nyashinki ambayo walikuwa wamehudhuria.

Katika juhudi za kuzima madai hayo Mutua alisema hakudhamiria kumuacha mkewe katika hali hiyo na kuomba msamaha.

vi) Nyota Ndogo kwa Henning Nielsen

Mwaka jana msanii mkongwe  Nyota Ndogo alijipata baada ya mumewe Henning Nielsen kutoka Denmark kukatiza mawasiliano naye kufuatia utani aliomfanyia.

Nyota Ndogo alihaha mitandaoni na mpaka kukata safari ya Ulaya katika juhudi za kumtafuta mumewe ili  kumuomba msamaha warudiane.

Baada mzungu huyo hatimaye alirudi Kenya na kuridhia msamaha wa Nyota Ndogo na wawili hao kurudiana.

vii) Frankie Just Gym It kwa Maureen Waititu na Corazon Kwamboka

Hivi majuzi mtaalamu wa mazoezi ya kujenga misuli Frankie Just Gym It alilazimika kuomba msamaha baada ya kutoboa siri za ndani kuhusu waliokuwa wazazi wenzake Maureen Waititu na Corazon Kwamboka.

Frankie alidai kuwa wapenzi hao wake wa zamani walikosa kielelezo cha baba katika maisha yao, jambo ambalo hapo awali waliwahi kuzungumza naye kulihusu.

Ufichuzi wa Frankie ulikumbana na ukosoaji mkubwa na hatimaye akakiri kuwa alikosea na kuwaomba msamaha wazazi wenzake.