Kwa muda mrefu kumekuwa na madai kwamba msanii Bahati ni mdogo kiumri kuliko mke wake Diana Marua, mpaka wengi wakambandika jina kuwa ni mtoto wa Diana ambaye ni mama wa watoto wake.
Msanii huyo sasa ameonekana kulikubali hilo asilimia mia kwa mia ambapo alisema kwamba ni kweli Diana Marua anamshinda kiumri kwa miaka mitatu na haoni tatizo katika hilo kwani kikubwa katika ndoa si umri bali heshima na amani.
Msanii huyo alisema kwamba yeye alikuwa amepitia shida nyingi katika maisha ya mitaa ya mabanda na ndio maana alikuwa anataka kuoa mwanamke mweney yuko mbele yake kiumri ili kumsaidia kumfunza maisha ya kuwa mwajibikaji.
“Kigezo cha umri hakikuwa tatizo kati yetu tulipokutana mara ya kwanza, na kama ambavyo ninasema hadharani kila mara ni kwamba ameniacha na miaka 3, lakini kwangu mimi nimepitia mengi maishani, nimeteseka sana kiasi kwamba akili yangu inakimbia sana. Ndio maana nilikuwa nataka kuoa mtu ambaye atakuwa mbele yangu kiumri ili pia mimi nijifunze mambo mengi kwa njia ya kuwa mtu anayewajibika na mambo kama hayo, hiyo ndio ilikuwa sababu,” msanii Bahati alifunguka ukweli wake kwa Dr. Ofweneke.
Msanii huyo alisema kwamab kikubwa kilichomvutia kwa Diana Marua ni kwamba yeye ni msichana mkubwa kwao na hivyo alikuwa tayari ashalea wadogo wake ndio maana pia akaona hata yeye anaweza kumlea vizuri.
“Diana alikuwa nyuma hapo amelea familia yake na wakati nilitaka kuanzisha familia, nilitaka mtu ambaye tukianzisha familia, nilitaka mtu ambaye anaweza kuniundia mazingira ambayo sikuwahi fanikiwa kupata katika maisha yangu awali kwa sababu mnajua mimi ni yatima,” Bahati alielezea.
“Nilitaka mtu ambaye anaweza nisaidia kujenga familia ya kiasili ili niweze kuhisi kitu ambacho nilikosa sana katika maisha ya utotoni, mimi hata sikujua vile wazazi hulea au hata sikuwahi kuijua sura ya mamangu,” Bahati aliongeza.
Msanii huyo pia alisema anamtambua na kummiminia sifa kochokocho msanii wa injili Guardian Angel kwa kufanya uamuzi wa kuoa mwanamke anayemzidi kiumri mara dufu.