Hadi sasa, muigizaji na mwanamitindo mashuhuri wa Bongo Wema Sepetu bado hajaweza kumshika mtoto toka tumboni mwake.
Kwa miaka mingi, mpenzi huyo wa zamani wa Diamond Platnumz amekuwa akishambuliwa na kukejeliwa mitandaoni kutokana na hali yake.
Takriban miaka minne iliyopita Wema aliwahi kufunguka kuhusu tatizo kwenye tumbo lake la uzazi linalomzuia kushika ujauzito.
“Unajua mimi nilikuwa na tatizo kubwa sana kwa upande wa tumbo langu la uzazi lililosababisha nisiweze kuzaa kwa muda wote huu. Ngoja niweke wazi leo watu wajue, mimi nina ugonjwa ambao unasababisha mayai yangu ya uzazi kutoboka na kushindwa kupevusha mbegu za uzazi," Alisema katika mahojiano na Global Publishers.
Licha ya kuwa na tatizo kwenye tumbo la uzazi, muigizaji huyo mwenye sauti nzuri kweli ameonyesha wazi kuwa bado hajapoteza matumaini ya kuwahi kukumbatia mtoto wake kuzaa katika siku za usoni.
Wema ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 31 amedokeza kuwa anatamani sana kupata mtoto wa kiume.
"Siku moja natamani kuwa na mtoto wa kiume. Kheri za siku ya kuzaliwa Baby Joel wa Lily Wangu," Wema alisema kupitia Instagram.
Miss Tanzania huyo wa mwaka wa 2006 alikuwa akimtakia kheri za siku ya kuzaliwa mtoto wa rafiki yake Lily Mawalla.
Miaka miwili iliyopita Wema akiwa katika mahojiano alisema moyo wake utapata amani na kutulia pindi tu atakapojaliwa mtoto wake.
"Linapokuja suala la mtoto na mimi, nahisi kiu yangu itaisha pale nitakapomshika wa kwangu na itaendelea kuniuma mpaka nitakapopata wangu, itaniuma mpaka kesho hadi kifo na kama Mungu amenijalia nisipate sawa hamna shida kwa hiyo nitaingia kaburini bila mtoto wangu bado nitaumia," Wema alisema katika mahosjiano na EATV.
Muigizaji huyo mwenye kipaji kikubwa hata hivyo hajakuwa bila uwezo wa kushika ujauzito katika miaka yote ya maisha yake.
Awali akiwa kwenye mahusiano na marehemu Steven Kanumba aliwahi kupata ujauzito mara mbili na kila mara kuutoa, jambo ambalo anaamini limemwathiri hadi wa leo.
Wema aliwahi kukikiri kuwa kuavya mimba ya kwanza ilikuwa ni makubaliano kati yao wawili ila ya pili ilifanywa kwa siri bila Kanumba kujua.