Mwimbaji mashuhuri Kevin Bahati baada ya kuoneshwa kivumbi katika kinyang’anyiro cha ubunge Mathare, sasa ameingia bafuni amejikosha na kurudi sokoni upya kabisa ambapo ameshikiri katika mahojiano yake ya kwanza kabisa tangu kukamilika kwa uchaguzi.
Safari hii ameshiriki mahojiano na mtangazaji maarufu kutoka Tanzania Millard Ayo.
Katika mahojiano hayo, Bahati ambaye alifichua kwamba Desemba mwaka huu anafikisha miaka 29 na ndoto yake kubwa ilikuwa ni kutaka kuwawakilisha watu wa mtaa uliomlea, Mathare bungeni ila ndoto hiyo sasa ni kama imefukizwa kabisa baaada ya kuibuka kwa mbali nambari tatu katika uchaguzi huo.
Pia alidokeza kwamba ndoto yake nyingine kabla kufika miaka 30 ilikuwa ni kuwa bilionea lakini sasa pia hiyo ni kama itakuwa tayari imeyeyuka ila akasema kwamba bado ndoto yake ya kuwa rais wa Kenya katika uchaguzi wa mwaka 2017 bado ipo na atazidi kuifanyia kazi katika kila sekunde iendayo kwa Mungu.
“Chukua neno langu. 2037 nitakuwa rais ajaye wa Kenya. Hiyo ndiyo ndoto yangu. Mimi ni mtoto wa Kenya, Ningependa pia Mungu akiniwezesha nisaidie Wakenya kwa jumla,” msanii huyo alifichua.
Akiulizwa kwa nini anawazia urais wakati tayari ubunge ushamtokea puani, mwanamuziki huyo alisema kwamba mnamo mwaka 2017 alipokuwa akitumbuiza katika moja ya hafla ya viongozi wa Jubilee wakiongozwa na rais Kenyatta, alipata kukalia kiti cha rais kwa sekunde za kuhesabu na jambo hilo liliotesha ndoto zake za kutaka kuwa rais siku moja Mungu akiendelea kumujaalia maisha na afya njema.
“Nadhani nilivunja rekodi kubwa sana hata kama sikua nimepanga. Niliinua rais, kisha nikakalia kiti chake nikimbia mama wa taifa. Niliona inawezekana. Ni kuwa tu na ndoto, unaiamini na kuifanyia kazi,” Bahati alisema.
Bahati alijitosa kwenye siasa mapema mwaka huu kuwania ubunge Mathare kupitia tikiti ya chama cha Jubilee ambayo ilikuja na masaibu si haba huku baadhi wakifanya kazi usiku na mchana kumfungia nje ya kinyang’anyiro hicho ila akasimama kidete na kuhakikisha jina lake limeona tundu la debe ila kwa bahati mbaya kama lilivyo jina lake basi bahati haikusimama upande wake kwani alimaliza nambari tatu kwa kura elfu nane na ushei nyuma ya Billian Ojiwa wa UDA aliyeibuka wa pili na mbunge wa sasa Anthony Oluoch wa ODM akakitetea kiti chake.