Mwanamke mmoja kutoka kaunti ya Homa Bay sasaanadai kwamba kulikuwepo na jina la mtu aliyehujumu uchaguzi mkuu wa Agosti tisa kwa jina ‘Opaque’ kama ilivyotajwa na makamishna wanne waliojitenga na matokeo ya uchaguzi wa urais na kusema kwamba huyo pia naye anafaa kushikwa na kufunguliwa mashtaka.
Wiki jana, neno hilo ‘Opaque’ lilizungumziwa sana mitandaoni baada ya naibu mwenyekiti wa tume ya IEBC Juliana Cherera kusema kwamba yeye na wenzake watatu walijitenga na matokeo aliyotangaza mwenyekiti Chebukati kumpa Ruto ushindi kutokana na hali ya utata (Opaque) iliyozingira mchakato huo haswa katika hatua zake za kileleni.
Baada ya watu wengi kuzungumzia neno hilo, sasa baadhi ya Wakenya wameibua mdahalo kulihusu huku wengine wakiwa sasa wameamini kwamba ‘Opaque’ ni jina la mtu mmoja miongoni mwa wale waliohujumu matokeo hayo kwa upendeleo wa naibu rais anayeondoka William Ruto.
Katika video hiyo, mwanamke huyo wa Homa Bay sasa anasema anamchukia William Ruto, mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati na huyo mwingine anayesema ni Opaque na kutaka wote watatu kuchukuliwa hatua za kisheria na kinidhamu.
“Chebukati alifanya kitu alikuwa anajua, mimi nachukia Chebukati, Opaque pamoja na Ruto mwenye alimnunua na pesa yake. Wote nawachukia. Chebukati ashikwe, Opaque ashikwe pamoja na Ruto aliyetumia pesa kuwahonga Opaque na Chebukati,” mwanamke huyo anafoka kwa hasira katika mkanda huo.
Jamaa mwingine pia katika video hiyo anayeonekaan kuamini Opaque alikuwa ni mtu anasema kwa maoni yake haoni kama kuna haja ya Opaque kushtakiwa kwani yeye alikuwa anataka tu pesa yake na kufanay kile alichoagizwa.
Jana muungano wa Azimio la Umoja One Kenya uliwasilisha shehena la Ushahidi katika mahakama ya upeo jijini Nairobi katika ombi lao la kutaka matokeo yaliyotangazwa na Chebukati kumpa Ruto ushindi kubatilishwa.