Mwimbaji na mjasiriamali mashuhuri Esther Akoth almaarufu Akothee kwa sasa amezama ndani kabisa kwenye dimbwi la mapenzi.
Msanii huyo mwenye umri wa miaka 42 yuko kwenye mahusiano na mwanamume mzungu wa umri wa makamo ambaye alimtambulisha siku chache zilizopita. Ni wazi kuwa mwanaume huyo sio mpenzi wake wa kwanza.
Katika miaka ambayo imepita Akothee amewahi kuwa kwenye mahusiano na wanaume kadhaa na hata kupata watoto na baadhi yao.
Sio maelezo yote ya maisha ya uchumba ya mwimbaji huyo ambayo yamewekwa hadharani lakini kuna baadhi ya mahusiano yake ya awali ambayo yanajulikana kuhusu hasa ambayo amekuwa nayo miaka ya hivi majuzi.
1. Akothee na Jared Otieno
Bw Jared Otieno ni mume wa kwanza wa Akothee na baba ya mabinti wake watatu wakubwa; Vesha Okello, Rue Baby na Fancy Makadia.
Wawili hao walikuwa kwenye ndoa kwa miaka mingi kabla ya kutengana mwaka wa 2006 na kila mmoja kuenda njia zake.
Mapema mwaka huu Akothee alifichua kuwa ilimchukua takriban miaka 6 kupona jeraha la moyo baada ya talaka yake kutoka kwa mpenzi huyo wake wa utotoni.
"Ilinichukua miaka 6 kupona na kusonga mbele kutoka kwa mshtuko na huzuni ya talaka. Nilijifunza kwamba hakuna kitu kilikuwa katika uwezo wangu isipokuwa maisha yangu na ya watoto wangu," alisema kupitia mtandao wa Instagram.
Pia aliwahi kufichua kuwa alitoroka nyumbani kwao na kuenda kuolewa na Jared akiwa na umri mdogo wa miaka 14 tu.
2. Akothee na Papa Ojwang'
Takriban mwongo mmoja baada ya kutengana na Jared, Akothee alitambulisha mzungu mmoja kutoka Uswizi kama mpenzi wake. Wawili hao walikaa pamoja kwa muda na hata kubarikiwa na mtoto mmoja wa kiume mwakani 2008.
Machache tu yanajulikana kuhusu baba huyo wa mtoto wa nne wa Akothee na ni wazi kuwa mwanamuziki huyo hapendi kumzungumzia. Kuonyesha uhusiano mbaya wa sasa kati ya wawili hao Akothee hata amembandika Papa Ojwang jina 'Baby daddy sumu!"
Hapo awali Akothee amewahi kufunguka jinsi alilazimika kurudi Kenya kutoka Uswizi takriban miaka kumi na minne iliyopita baada ya Papa Ojwang kumfukuza akiwa na ujauzito wa miezi tisa. Mpenzi huyo wake wa zamani alidai kuwa hakuwa tayari kuwa na mke ndiposa akamfukuza.
"'Rudi Afrika sina nguvu wala familia ya kutunza mwanamke mjamzito, siko tayari hata kuwa na mke' alisema baba mtoto wangu 👏💪," Akothee alisimulia.
3.Akothee na Papa Oyoo
Baada ya kutengana na Papa Ojwang', Akothee alikutana na mzungu mwingine kutoka Ufaransa, Dominic, na kujitosa kwenye mahusiano naye. Wawili hao walichumbiana kwa miaka kadhaa kabla ya kutengana mwaka wa 2013.
Katika kipindi cha mahusiano yao Akothee alipata ujauzito wa Bw Dominic na kujifungua mtoto wa kiume ambaye alipatia jina Oyoo.
4. Akothee na Nelly Oaks
Nelly Oaks alikuwa meneja wa Akothee kabla ya kupanda cheo na kuwa mpenzi wake. Wawili hao walifichua mahusiano yao mwaka jana.
Mapenzi kati ya wawili hao hata hivyo hayakudumu kwani walitengana miezi kadhaa tu baada ya kutangaza mahusiano yao. Akothee alithibitisha kutengana kwake na Bw Oaks mwezi Juni kupitia ukurasa wake wa Instagram.
"Nimetoka kwenye mahusiano mengine yenye misukosuko tofauti, kwa hivyo hii ya mwisho isiwe ya kushtua au ya kushangaza... Ni uamuzi wa kibinafsi, nahitaji muda wa kuzingatia furaha yangu mpya niliyopata na uharibifu mdogo, ninahitaji kujishughulisha mwenyewe na kazi yangu, siko tayari kwa ahadi yoyote," alitangaza.
5. Akothee na Mpenziwe wa sasa
Hivi majuzi Akothee alimtambulisha mpenzi wake mpya mzungu. Ni maelezo machache tu yanayojulikana kuhusu mpenzi mpya wa mwimbaji huyo.
Mama huyo wa watoto watano alifichua sura ya mzungu huyo mwenye umri wa makamo ila hakufichua jina lake wala nchi yake ya kuzaliwa.
Akothee ameonekana kufurahia mahusiano yake mpya na tayari amedokeza kuwa huenda akafunga pingu za maisha na mzungu huyo.
"Sikujua kijiji changu kingeweza kuwa Paradiso. Mfalme alikuwa akikosekana. Sasa naweza kusema maisha yangu yamekamilika na niko tayari kutulia, niko tayari kuwa mke mtiifu," Akothee alisema hivi majuzi.