Msichana mdogo alizua vichekesho mitandaoni baada ya video kumuonesha akibishana vikali na makanga wa matatu aliyoiabiri.
Msichana huyo ambaye alikuwa amevalia sare za shule alikuwa ameabiri gari hilo na alipofika pa kushukia ili kuingia shuleni, kondukta alimuitisha nauli, hapo ndipo msichana huyo mdogo aliota pembe na kumpa makanga mzomo huku akisema hata senti moja hatoi mfukoni.
Klipu hiyo iliibua vichekesho vingi kwenye mtandao wa TikTok ambapo wengi walishangazwa na ujasiri wa mtoto huyo mdogo ambaye alimsimamia tisti manamba na kumpa makavu moja kwa moja kuwa hawezi lipa nauli.
Manamba huyo alionekana kumshikilia mkono kama njia moja ya kumshrutisha kulipa nauli huku watu kadhaa wakiwa wamejaa eneo hilo ambalo mtoto mdogo wa shule alizua tafrani.
Mtoto huyo anasikika akiteta vikali kumwambia makanga kuachilia mkono wake huku msimamo wake ukiwa pale pale kwamba hangetoa hata shilingi.
Msichana huyo alijitetea kwamba hatua yake ya kutotoa nauli ni kutokana na makanga kumuahidi kumshusha katika eneo ambalo angefika shuleni kwa urahisi ila kwa bahati mbaya au tuseme usahaulifu, gari likampitisha na kumshusha binti huyo kituo cha mbele.
Kondakta alikasirika na kusema kwamba angemweka ndani ya buti ya basi ikiwa hatamlipa. Akiwa bado anaongea, kondakta alimuinua lakini kwa watazamaji kuingilia kati, hakuweza kutekeleza mpango wake. Msichana huyo mdogo baadaye aliondoka eneo la tukio bila kulipa nauli na baadhi ya wanamtandao walimshangilia kwa uhodari wake.
“Tazama aina ya ujasiri alionao anajua haki yake hakuna anayefaa kumdanganya hata mwanafunzi mwenzake ataenda kukusanya woto woto kama watafanya kwa vyovyote vile,” mtumizi mmoja wa Tiktok aliandika.
“Hapa panaitajika upako wa Yesu kuingilia kati kama mwanafunzi mdogo anaweza kuwa na ukali kama huu, hawezi kubali kulaghaiwa kamwe. Mtoto mdogo mwenye akili ya watu wazima,” mwingine alistaajabu.