Mwanasoshalaiti Faith Makau almaarufu Amber Ray hakuwahi kuwa kwenye mahusiano ya kimapenzi na mwimbaji Brown Mauzo, Vera Sidika alidai.
Katika mahojiano na Massawe Japanni, Vera alidai mahusiano yanayodaiwa kuwahi kutokea hapo awali kati ya mumewe na Amber Ray ilikuwa ni kiki tu.
Mwanasoshalaiti huyo aliweka wazi kuwa mumewe tayari alikuwa kwenye mahusiano mengine wakati ilipodaiwa anachumbiana na Amber Ray.
"Wakati wa mahusiano yake ya awali, alikuwa akifanya kiki na mtu maarufu (Amber Ray). Hiyo kiki ikifanyika alikuwa kwenye mahusiano," alisema.
Mnamo 2019, Mauzo na Amber Ray walidai kwamba walikuwa wakichumbiana. Wawili hao waliweka 'mahusiano' yao kuwa siri lakini walikuwa wakichapisha picha zilizoonyesha wakiwa kwenye likizo, madukani na hata wakijivinjari pamoja.
Mahusiano hayo yalikuja miezi kadhaa baada ya Amber Ray kuachana na aliyekuwa mpenzi wake na wakati ambapo Brown Mauzo alikuwa akivuma kufuatia picha iliyoonyesha akijivinjari na mwimbaji Akothee.
Miezi michache iliyopita Amber Ray alikana kuwahi kutoka kimapenzi mume huyo wa mwanasoshalaiti mwenzake Vera Sidika.
Katika kipindi cha maswali na majibu kwenye Instagram, mama huyo wa mvulana mmoja alisema kilichokuwa kati yao kilikuwa ni kiki tu.
Kuhusu iwapo yeye na Mauzo walichumbiana, alikanusha madai hayo na kusema kwamba ilikuwa ni njia ya kuwinda shoo.
Katika kipindi hicho shabiki mmoja alimuuliza, "Ulitoka na Mauzo kweli au ilikuwa showbiz??"
"Showbiz 100%, hatujawahi hata kubusu," alisema.
Katika mahojiano, Vera alifichua kuwa mahusiano ya mumewe na baby mama wake yalidumu kwa takriban miezi 10 kabla ya kuvunjika hatimaye.
"Wakati tulipokutana, alikuwa ameachana na ex wake kama miezi 8 iliyokuwa imepita, walikuwa kwenye mahusiano kwa miezi 10," alisema.
Mama huyo wa binti mmoja alifichua kuwa Mauzo alikuwa kwenye mahusiano yake ya awali walipokutana mara ya kwanza kabla kuchumbiana.
Wakati wanandoa hao walipokutana kwa mara ya kwanza takriban miaka mitatu iliyopita, Vera pia alikuwa kwenye mahusiano mengine na hata alikuwa pamoja na mwanaume ambaye alikuwa akichumbiana naye wakati huo.
"Baadae tulikutana nikiwa single na yeye akiwa single," alisema.
Wawili hao kisha walijitosa kwenye uhusiano wa kirafiki kwa miezi kadhaa kabla ya kuanza kuchumbiana.
Baada ya kuwa kwenye urafiki kwa muda na kufunguka kuhusu maisha yao, Vera aligundua kuwa mwimbaji huyo ni mwanaume tofauti.
"Niliona ni mtu tofauti. Brown hata hajawahi kunywa pombe. Tulikuwa tunapigiana simu na kuongea kutoka saa tatu usiku mpaka saa kumi na moja asubuhi. Tulikuwa marafiki. Tulikuwa wazi sana," alisema.