Mwimbaji wa nyimbo za Injili , Daddy Owen amefichua kuwa hajashiriki tendo la ndoa kwa miaka miwili.
Katika mahojiano yake na mwanahabari, Owen alisema kuwa hajakuwa na hamu ya kufanya mapenzi kutoka pale walipotengana na mke wake.
"Sihitaji mwanamke, sijafanya mapenzi kwa miaka miwili, mwanamke ni wa kazi gani?" Owen alisema.
Haya yalijiri mwimbaji huyo alipofichua kuwa hataki mwanamke kwenye maisha yake tena hata baada ya kutangaza kuwa anatafuta mke.
Alisema kuwa amegoma kutafuta mwanamke ambaye alikuwa amesisitiza anataka kuoa wa kijijini.
"Sitaki hata kupikiwa, nitakula hotelini, hata wageni wakija nyumbani kwangu tutanunua chakula, sitaki kuoa tena," mwimbaji huyo alisema.
Alisema kuwa ametosheka na maisha yake sasa hivi na kuwa ana mambo mengi ya kufanya si kutafuta mke wa kuoa.
Owen aliongeza kuwa anafurahia maisha yake ya kuwa singo kwa wakati huu.
"Kwa sasa nafanya mambo mengi, sitafuti tena mke. Nitafute mke wa nini? Kama ni mtoto ninaye tayari, si bora kuwa na mtoto," Owen alisema.
"Mwanaume akifika miaka fulani anahisi kuwa ametosheka na yale ako nayo, nina mtoto na nimetosheka na hayo . Nilishaoa kitambo na haikufaulu, niko sawa hivi," baba huyo wa watoto wawili alisema.
Hivi majuzi, mwimbaji huyo alikuwa ametangaza kuwa anatafuta mke wa kuoa na kusisitiza kuwa anataka tu msichana wa kijijini.
Daddy Owen na mkewe Farida Wambui walitengana baada ya miaka minne ya ndoa. Kisa chao kilisambaa mnamo 2020 baada ya kubainika kuwa mkewe alikuwa amechumbiwa na tajiri wa Kenya.