Mwanamitindo maarufu wa Tanzania Paula Kajala amewatambua wazazi wake Kajala Masanja na P-Funk Majani.
Siku ya Jumanne, kipusa huyo mwenye umri wa miaka 20 alichapisha picha ya kumbukumbu ya wazazi hao wake ambayo ilipigwa takriban miongo miwili iliyopita wakati walipokuwa kwenye mahusiano.
"❤🤘❤," aliandika chini ya picha hiyo ambayo alipakia Instagram.
Pichani, P-Funk anaonekana akimbusu mchumba huyo wa sasa wa Harmonize kwenye shavu la kulia. Wawili hao wanaonekana wamekaa kwenye studio ya picha.
Kwenye picha hiyo Kajala anaonekana mwenye furaha sana, pengine akifurahia siku hizo nzuri za zamani wakati penzi lao lilipokuwa limetaradadi.
Paula pia alisherehekea familia ya sasa ya babake. Alichapisha picha iliyomuonyesha akifurahia muda na Bw Majani, mkewe SamiraMollel na watoto wao watatu.
Aidha alichapisha picha ya Bi Samira na kuwaomba wanamitandao kufuatilia ukurasa wake mpya wa Instagram. Katika ujumbe wake kwa wanamitandao, mwanamitindo huyo alimtambua Bi Samira kama mama yake.
"Tafadhali fuatilieni akaunti mpya ya mama yangu @sameeramollel. Akaunti yake mzee ilidukuliwa," aliandika.
Licha ya wazazi wake kutengana miaka mingi iliyopita, siku za hivi majuzi Paula amekuwa na uhusiano wa karibu na familia ya babake.
Takriban miezi minne iliyopita, mwanamitindo huyo aliweka wazi kuwa kuna uhusiano mzuri kati yake na Bw P-Funk Majani.
Paula alifichua kwamba huwa anawasiliana na mtayarishaji huyo wa muziki na hata kuonana naye mara kwa mara.
"Tuko sawa. Kila siku tuko sawa. Tunaongea. Hata nilikuwa napanga kuenda kwake wiki iliyopita. Anakaa Arusha sasa hivi," Paula alisema katika mahojiano na Wasafi Media.
Alifichua kuwa huwa anatembelea familia ya mzazi huyo wake na kubainisha kuwa kuna uhusiano mzuri kati yake na wadogo zake kutoka upande huo.
"Huwa tunaongea. Tunafanya video call. Tunazungumza. Huwa tunakutana mara nyingi. Hata nilikuwa naishi nao," alisema.
Mapema mwaka huu, Majani pia aliwahi kufunguka kuhusu uhusiano wake na bintiye huyo wake na kuweka wazi kwamba huwa wanajuliana hali mara kwa mara na hata kukutana kwa wakati mwingine.
Baba huyo wa watoto wanne hata hivyo alifichua kuwa hakuna uhusiano mzuri kati yake mamake Paula, Kajala Masanja.
Majani alidai kuwa mchumba huyo wa sasa wa Harmonize amekuwa akipuuzilia ushauri wake hasa kuhusu malezi ya binti yao.
"Paula bado mdogo, ana nafasi ya kubadilisha tabia. Mama yake yule hapana. Kwa kweli sisi hatuongei. Sihitaji kuongea naye tena!," Alisema.
Pia aliweka wazi kuwa kwa muda mrefu hakujakuwa na hali ya kuelewana kati yake na Kajala.na kufichua kuwa kwa sasa hata hazungumzi naye.
"Mama (Kajala) ni sumu. Lazima izingatiwe niko kwenye ndoa miaka nane na mtu ambaye nimekuwa naye miaka 12, kanizalia watoto watatu. Sasa kama mtu ako na drama unaepuka kidogo," P-Funk alisema.