Diamond aonyesha upendo mkubwa kwa mzazi mwenza wake Zari Hassan

Diamond alichapisha bango la tangazo la shoo hiyo na kuwahimiza Waganda kujitokeza.

Muhtasari

•Diamond alitumia ukurasa wake wa Instagram wenye wafuasi zaidi ya milioni 15.5 kutangaza shoo ya 'Zari The Boss Lady All White Party'.

•Diamond pia ameandaa shoo kubwa ya kufunga mwaka pamoja na msanii wake Zuchu ambayo itafanyika mnamo mkesha wa mwaka mpya.

Zari Hassan ,Diamond Platnumz na watoto wao Tiffah na Nillan.
Image: HISANI

Bosi wa WCB Diamond Platnumz kwa mara nyingine ameonyesha upendo mkubwa kwa mzazi mwenzake mwanasoshalaiti Zari Hassan.

Siku ya Jumatano, staa huyo wa Bongo alitumia ukurasa wake wa Instagram wenye wafuasi zaidi ya milioni 15.5 kutangaza shoo ya 'Zari The Boss Lady All White Party' ambayo imeratibiwa kufanyika leo Alhamisi usiku.

Diamond alichapisha bango la tangazo la shoo hiyo na kuwahimiza Waganda kujitokeza kwa wingi .

"Usiku wa kukumbuka!! ZARI ALL WHITE PARTY 2022 Kesho jijini KAMPALA UGANDA!!" aliandika chini ya bango hilo.

Shoo hiyo itafanyika katika jiji kuu la Uganda, Kampala na mdhamini mkuu ni Belaire. Tikiti zinauzwa kutoka shilingi 75,000 za Uganda hadi 4M.

Zari na mpenzi wake wa sasa Shakib Cham Lutaaya wamekuwa wakiitangaza sana shoo hiyo ambayo wanatarajiwa kuandaa pamoja.

Diamond pia ameandaa shoo kubwa ya kufunga mwaka pamoja na msanii wake Zuchu ambayo itafanyika mnamo mkesha wa mwaka mpya.

Hivi majuzi umekuwa na tetesi kuwamastaa hao wa Bongo ambao wanadaiwa kuwa wapenzi wanapanga kufunga pingu  za maisha siku hiyo.

Mwishoni mwa mwezi Novemba, Zari Hassan alikuwa amedokeza kwamba atakuwa nchini Tanzania katika msimu wa Krisimasi.

Mwanasoshalaiti huyo mzaliwa wa Uganda alishiriki mazungumzo ya simu na Mama Dangote ambapo alimthibitishia kuhusu ziara hiyo ya Desemba. Alimwambia mzazi huyo wa Diamond kwamba atawapeleka wajukuu wake Tiffah Dangote na Prince Nillan ili waweze kufurahia muda na wanafamilia wengine.

Katika mazungumzo hayo, Zari ambaye kwa sasa anaishi na familia yake Afrika Kusini alidokeza kuwa mpango wa kusherehekea sikukuu ya Krismasi nchini Tanzania ni uamuzi ambao alifanya pamoja na Diamond.

"Baba yao amesema wanakuja Krismasi. Bado tuko shule," Zari alimwambia Mama Dangote katika mazungumzo.

Ikitokea, hii haitakuwa mara ya kwanza kwa Zari Hassan na watoto wake kutembelea familia ya kina Diamond katika miaka ya hivi majuzi. Mfanyibiashara huyo mwenye umri wa miaka 42 bado huwa anatembea nyumbani kwa mzazi huyo mwenzake licha ya wao kutengana takriban miaka minne iliyopita.

Mara nyingi anapozuru Tanzania, mama huyo wa watoto watano huwa ameandamana na watoto wake na Diamond, Tiffah na Nillan. Yeye na watoto hao wake wadogo wamehifadhi uhusiano mzuri na familia ya staa huyo wa Bongo licha ya tofauti zilizotokea hadi kuvunja mahusianoi yao ya muda mrefu.

Hata hivyo, kulikuwa na tetesi kuwa mwanasoshalaiti huyo alipanga ziara hiyo baada ya Diamond na Zuchu kutangaza mahusiano yao. Baadhi walidai kuwa anapanga kuvuruga mahusiano ya wawili hao.