"Ni uchungu sana!" Stivo Simple Boy avunja kimya kuhusu kifo cha babake

Msanii huyo aliwataka mashabiki kumuombea na kumpa nguvu akimuomboleza babake.

Muhtasari

•Stivo alidokeza kuwa inauma sana kumpoteza mzazi huyo wake na kuwaomba mashabiki kuendelea kusimama naye.

•Mwanamuziki huyo ni mzaliwa wa saba katika familia ya watoto wanane.

Stivo Simple Boy
Image: HISANI

Rapa mashuhuri Stephen Otieno Adera almaarufu Stivo Simple Boy amethibitisha kifo cha baba yake Anthony Adera.

Akizungumza kupitia mitandao ya kijamii siku ya Jumatatu asubuhi, msanii huyo kutoka Kibra alidokeza kuwa inauma sana kumpoteza mzazi huyo wake na kuwaomba mashabiki kuendelea kusimama naye.

"Ningependa kuwaambia mashabiki wangu kwamba nimepata msiba ya kupoteza babangu mzazi Anthony Adera. Ni uchungu sana kupoteza mzazi ila naomba mniombee na mnisapoti kwa huu wakati mgumu," alisema.

Stivo aliwataka mashabiki wake kumuombea na kumpa nguvu huku akiendelea kumuomboleza baba yake mpendwa.

Habari kuhusu kifo cha babake Stivo, Anthony Adera zilifichuliwa na wasimamizi wake wa muziki mnamo Jumapili asubuhi.

"Ni kwa majuto na huzuni kwamba tunatangaza kifo cha Anthony Adera, baba yake Stephen Otieno Adera anayejulikana kama Stevo Simple Boy," wasimamizi Men In Business (MIB) walitangaza kupitia taarifa.

MIB walitoa wito kwa mashabiki wa msanii huyokutoka Kibra kusimama naye kwa maombi katika kipindi hiki kigumu cha maisha yake.

“Taarifa zaidi zitawasilishwa,” taarifa ilisoma.

Wazazi wa Stivo wanatokea Oyugis katika Kaunti ya Homabay ambapo mwanamuziki huyo wa nyimbo za kufoka alizaliwa na kukulia kabla ya kuhamia jijini Nairobi baada ya kumaliza elimu ya Shule ya Msingi.

Mwezi Julai mwaka jana, msanii huyo alifichua kuwa aliwajengea wazazi wake nyumba kijijini hapo baada ya shoo na dili zilizofanikiwa.

Alifichua kuwa aliwajenga  wazazi wake  kwa kutumia pesa alizopokea alipokuwa akifanya kazi na usimamizi wake wa zamani.

“Nilipokea nusu milioni katika tangazo la dau la Odi. Nilitumia pesa hizo kuwajengea wazazi wangu nyumba,” Stivo Simple Boy alisema.

Mwanamuziki huyo ni mzaliwa wa saba katika familia ya watoto wanane.