"Watoto wangu kuwa hai ni muujiza mkubwa" Size 8 afunguka mapambano ya kuzaa watoto

Size 8 alidokeza kwamba angekuwa bila mtoto kama si muujiza wa Mungu.

Muhtasari

•Size 8 alibainisha kuwa wawili hao bado kuwa hai na wenye afya njema ni muujiza mkubwa uliofanywa na Mwenyezi Mungu.

•"Mungu ulisimama penye pengo na kunipa ushindi. Haleluya tunalihimidi jina la Bwana," alisema.

Mwanamuziki Size 8 pamoja na familia yake.
Image: INSTAGRAM// SIZE 8

Mwimbaji wa nyimbo za Injili Linet Munyali almaarufu Size 8 amewasherehekea watoto wake wawili, Ladasha Belle Muraya na Muraya Jr na kumshukuru Mungu kwa ajili yao.

Akizungumza kupitia mtandao wa kijamii siku ya Jumapili, Mtumishi wa Mungu huyo aliyepakwa mafuta alidokeza kuwa kuna hadithi kubwa nyuma ya yeye kujifungua watoto wake ambayo sio wengi wanaifahamu.

Size 8 alibainisha kuwa wawili hao bado kuwa hai na wenye afya njema ni muujiza mkubwa uliofanywa na Mwenyezi.

"Lo! moyo wangu umejaa shukurani kwa Mungu aliye juu sana Baba yangu kupitia Yesu Kristo kwa uweza wake maishani mwangu. Si wengi wanajua hadithi yangu inapokuja suala la kuzaa watoto lakini wachache wanaojua hadithi za watoto hawa wawili wanajua kuwa wao kuwa hai ni muujiza mkubwa wa Mwenyezi Mungu," alisema kwenye Instagram na kuambatanisha ujumbe wake na video ya wanawe wakicheza.

Mwimbaji huyo wa zamani wa muziki wa kilimwengu alidokeza kwamba angekuwa bila mtoto kama si muujiza wa Mungu.

"Mungu ulisimama penye pengo na kunipa ushindi. Haleluya tunalihimidi jina la Bwana," alisema.

Size 8 ana watoto wawili na mumewe DJ Mo, wa kwanza, msichana Ladasha Belle mwenye umri wa miaka saba na Muraya Jr ambaye ana miaka minne.

Mwaka wa 2021, mwanamuziki huyo alipoteza ujauzito wa ambaye angekuwa mtoto wao wa tatu kutokana na shinikizo la damu.

Katika mazungumzo ya mwaka jana, alifichua kwamba amekuwa akipambana na shinikizo la damu zaidi ya miaka mitano iliyopita.

Ugonjwa wa Size 8 ulitambulika baada yake kuzirai mtaani alipokuwa anaelekea nyumbani baada ya kutumbuiza katika tamasha ambayo alikuwa amehudhuria pamoja na mume wake, DJ Moh.

"Nilizirai nikiwa mjini nikapelekwa katika hospitali moja iliyokuwa pale. Hapo ndipo nikaambiwa shinikizo la damu yangu ni kubwa mno. Nilikuwa siko sawa. Kutoka siku hiyo nilianza kuchukua dawa za shinikizo la damu," Size 8 alisimulia kupitia YouTube channel ya 'The Murayas'

Mama huyo wa watoto wawili alisema ugonjwa huo ulikuwa ukimzidia mara kwa mara na kumfanya alazwe hospitali mara kadhaa tangu ulipogunduliwa.

Alisema amekuwa akipambana nao kwa ujasiri. Hata hivyo alikiri kwamba hivi majuzi ugonjwa huo ulikuwa umemwathiri kiasi cha kupatwa na msongo wa mawazo na kutaka kukata matumaini ya maisha.

"Mara hii haikuwa rahisi kwangu. Nilihisi nilikuwa nazama kwenye msongi wa mawazo.Kama sio neema ya Mungu nadhani ningekufa moyo kabisa.. Nilihisi kama kwamba nimechoka kupambana, nimechoka kuendelea, nimechoka kusubiri, nimechoka kusubiri muujiza. Mara nyingi sikuwa nahisi vizuri. Kuna wakati Moh alikuja katika chumba cha malazi na nikamwambia sihisi poa na nahisi kukata tamaa. Hiyo ni baada ya kutoka hospitali. Tulishiriki naye mazungumzo marefu," Alisema.

Size 8 alisema mume wake amekuwa guzo muhimu katika mapambano yake na shinikizo la damu. Alisema Mo amekuwa akimtia moyo na kumsihi asikate tamaa.