"Mimi sio malaika!" Chameleone avunja kimya baada ya kumpiga viboko mwendesha bodaboda

"Mimi sio malaika, na mtu wa boda pia sio malaika," alisema.

Muhtasari

•Mwimbaji  huyo wa kibao 'Valu Valu' alisema tasnia ya boda boda pia ina watu wabaya.

•Aliomba msamaha kwa mashabiki wake, na kuahidi kushughulikia hali kama hizo kwa njia bora.

Image: INSTAGRAM// JOSE CHAMELEONE

Mwimbaji wa Uganda Jose Chameleone amesema kuwa yeye si mkamilifu baada ya video yake akimchapa viboko mwendesha bodaboda kusambaa mtandaoni wiki iliyopita.

Akizungumza na vyombo vya habari vya Uganda siku ya Jumatatu, mwimbaji  huyo wa kibao 'Valu Valu' alisema tasnia ya boda boda pia ina watu wabaya.

"Mimi sio malaika, na mtu wa boda pia sio malaika," alisema.

Mke wa zamani wa Chameleone, Danielle Atim alidai haki kwa mwendesha bodaboda aliyepigwa na mwimbaji huyo, na kuongeza kuwa hakuna mtu asiyeweza kushtakiwa.

"Hakuna kuruhusu vurugu," Atim aliandika kwenye Instagram, akinukuu mchoro uliosomeka: "Vurugu hazitavumiliwa."

Timu ya mawasiliano ya umma ya Chamelleone  pia ilitoa taarifa kuhusu tukio hilo, ikisema alimpiga mwendesha bodaboda huyo ili kujilinda.

Alidai kuwa mwendesha bodaboda huyo aliharibu upande wa kushoto wa gari lake aina ya Range Rover.

Aliomba msamaha kwa mashabiki wake, na kuahidi kushughulikia hali kama hizo kwa njia bora.

"Tukio hilo ni la kusikitisha na lingeweza kuepukika. Matukio kama hayo yatashughulikiwa vyema zaidi," Chameleone alisema kupitia timu yake ya PR.