"Mke wangu alifanya hivi" Juliani ajivunia ukulima wa mke wake Lilian Ng'ang'a

Juliani ameonyesha baadhi ya kazi za ukulima za mke wake Lilian Nganga.

Muhtasari

•Juliani alichapisha video fupi ya bustani yao ambapo Bi Lilian amepanda aina mbalimbali za mimea ya chakula kuanzia michicha, sukuma wiki, nyanya, vitunguu na kadhalika.

•Wawili hao walifunga pingu za maisha mapema mwaka uliopita kabla ya kubarikiwa na mtoto wa kiume mwezi Agosti.

Lilian Ng'ang'a na Juliani
Image: INSTAGRAM// JULIANI

Rapa  mashuhuri Julius Owino almaarufu Juliani ameonyesha baadhi ya kazi za ukulima za mke wake Lilian Nganga.

Siku ya Jumanne, mwimbaji huyo alichapisha video fupi ya bustani yao ambapo Bi Lilian amepanda aina mbalimbali za mimea ya chakula kuanzia michicha, sukuma wiki, nyanya, vitunguu na kadhalika.

Kwenye video hiyo, alionyesha fahari kubwa katika kazi nzuri ya mke wake.

"@ngangalilian #Wanawake katika Ukulima, Mke wangu alifanya hivi," alisema.

Mnamo mwezi Oktoba mwaka jana, Lilian alidokeza kurejelea kazi yake ya usimamizi wa miradi baada ya kuwa katika mapumziko ya miezi kadhaa ili kuangazia kujifungua na ulezi wa mtoto wao mdogo, Utheri.

Juliani na Lilian walitangaza mahusiano yao Septemba 2021, wiki chache tu baada ya Alfred Mutua na Mama Machakos huyo wa zamani kutangaza kutengana kwao baada ya kuwa pamoja kwa takriban mwongo mmoja.

Wawili hao walifunga pingu za maisha mapema mwaka uliopita kabla ya kubarikiwa na mtoto wa kiume mwezi Agosti.

Mwaka jana, Juliani alifichua kwamba alikuwa amekata tamaa ya kuchumbiana wakati ambapo alikutana na Lilian Ng'ang'a.

Akiwa kwenye mahojiano katika kituo kimoja cha redio cha hapa nchini, baba huyo wa watoto wawili alifichua kuwa wakati huo alikuwa akijiangazia mwenyewe na hakutaka chochote kuhusu wanawake.

"Nilikuwa celibate wakati huo ata sikutaka stori ya manzi ju nilikuwa mahali poa sana. Lakini vitu vilichukua mkondo tu vile inafaa," alisimulia.

Juliani alisema alikutana na mpenzi huyo wa zamani wa aliyekuwa gavana wa Machakos Alfred Mutua mwaka wa 2021 bila mpango.

Alibainisha kuwa hakuwa akitafuta mchumba wakati huo ila baada ya kuwa marafiki kwa muda wakajipata kwenye mahusiano.

"Baadae aliniambia kusema kweli hivi ndio kuko, mimi siko hapo. Mimi nilisema sikuwa najua nilidhani sisi ni mabeshte tu," alisema.

Mwimbaji huyo wa nyimbo za kufoka alitupilia mbali madai kuwa aliiba mke wa waziri wa masuala ya Kigeni, Alfed Mutua.