Mkewe King Kaka abubujikwa machozi akikumbuka kipindi alikuwa mgonjwa sana

Nana Owiti alifichua kuwa mumewe alikuwa dhaifu sana wakati picha hiyo ilipigwa.

Muhtasari

•Bi Owiti alichapisha picha moja ya kumbukumbu ya mwanamuziki huyo akiwa ameketi kwenye kiti huku akiitazama simu yake na kuonekana mwenye mawazo sana mara tu baada ya kutoka hospitalini.

Image: INSTAGRAM// KING KAKA

Mtangazaji Nana Owiti amekumbuka kipindi ambapo mume wake King Kaka alikuwa amekumbwa na ugonjwa mbaya.

Siku ya Alhamisi, Bi Owiti alichapisha picha moja ya kumbukumbu ya mwanamuziki huyo akiwa ameketi kwenye kiti huku akiitazama simu yake na kuonekana mwenye mawazo sana mara tu baada ya kutoka hospitalini.

Alifichua kuwa mumewe alikuwa dhaifu sana wakati picha hiyo ilipigwa na walikuwa wakihangaika kutafuta matibabu.

"Tulikuwa tumetoka hospitalini hapa kwa hivyo unavyoweza kufikiria, siku na usiku kabla ya hii zilikuwa ndefu zaidi.. King Kaka hakuweza kukaa kwenye kiti hiki kwa dakika tatu tu. Mifupa yake ilikuwa dhaifu," alisema.

Katika picha hiyo, shati na kofia za King Kaka zilionekana kutomtoshea kutokana na uzito mkubwa wa mwili aliokuwa amepoteza.

Bi Owiti amefichua kuwa rapa huyo alikuwa akivalia kofia na barakoa ili kuficha masaibu aliyokuwa akipitia wakati huo.

"Alitaka kuepuka maswali na kukaa kawaida," alisema.

Mtangazaji huyo alikiri kwamba ni kwa neema zake Mungu mumewe aliweza kupata afueni na kuondoka katika hali hiyo mbaya.

"Jamani! Sijui kukuhusu lakini najua Mungu yupo kwa sababu tulihisi upendo wake, aligusa mikono yetu na tuliona uso wake kwa wakati wake mwenyewe," alisema.

Owiti alitumia fursa hiyo kuwatia moyo watu wengine wanaopitia hali ngumu maishani na kuwataka wasipoteze matumaini.