Samidoh akumbuka usiku ambao Mike Sonko alimuunganisha na Karen Nyamu

"TBT na Mike Sonko & Moses Kuria jijini Dubai,"

Muhtasari

•Samidoh alichapisha video ya kumbukumbu ya tamasha lake la Dubai ambapo inaaminika kuwa alipata kukutana na mzazi mwenzake Karen Nyamu.

•Mike Sonko alifichua kwamba yeye ndiye aliyemuunganisha Samidoh na  seneta wa kuteuliwa, Karen Nyamu.

Mike Sonko, Karen Nyamu, Samidoh
Image: FACEBOOK

Siku ya Wapendanao, staa wa Mugithi Samuel Muchoki almaarufu Samidoh alichapisha video ya kumbukumbu ya tamasha lake la Dubai ambapo inaaminika kuwa alipata kukutana na mzazi mwenzake Karen Nyamu.

Samidoh alikuwa akitangaza shoo yake ya Jumanne usiku katika kilabu ya Mike Sonko ya Mombasa alipokumbuka usiku ambao gavana huyo wa zamani alihudhuria tamasha lake akiandamana na Waziri wa Biashara, Moses Kuria.

"TBT na Mike Sonko & Moses Kuria jijini Dubai. Tunarudia hii kitu leo pale Volume VIP Club- Shanzu, Karibuni!!" alisema kwenye video hiyo.

Takriban miezi minne iliyopita, Sonko alifichua kwamba yeye ndiye aliyemuunganisha Samidoh na  seneta wa kuteuliwa, Karen Nyamu.

Gavana huyo wa zamani alidai kuwa  aliwaunganisha wazazi wenza hao katika hafla ya Mugithi Night iliyofanyika Dubai miaka kadhaa iliyopita. Sonko alikuwa akitoa maoni chini ya chapisho  la Nyamu kwenye Facebook wakati alipotoa ufichuzi huo.

"Mnafaa mniitie chai. Mimi ndio nilikupea Samidoh pale Dubai nikiwa na Moses Kuria wakati wa Mugithi night," alimwambia Karen.

Karen ambaye kwa sasa ana watoto wawili pamoja na Samidoh hakupinga kauli hiyo na badala yake akamuomba asifichue zaidi.

"Mdosi malizia tu hapo usitoe video," alimjibu Sonko.

Katika video ambayo ilichapishwa na Samidoh kwenye mitandao ya kijamii, Sonko alimpongeza staa huyo wa Mugithi na kutumia fursa hiyo kuwaomba Wakenya wanaoishi Ughaibuni kusaidia familia zao nyumbani.

"Sisi tumekuja leo kumsikiliza Samidoh. Nawashukuru nyote kwa kualika Samidoh. Kwa sababu tulikuwa Dubai tukasema tukuje. Sisi kule Kenya tunategemea nyinyi watu Diaspora kwa sababu ya uchumi wetu. Tafadhali msisisahau ndugu zetu na mama zetu kule nyumbani. Tunaongoza nchi vizuri," alisema.

Katika mahojiano ya hapo nyuma na Radio Jambo, Karen alifunguka kuhusu kukutana kwake kwa mara ya kwanza na msanii huyo ambapo baadae alipakia video iliyoonyesha wakijivinajiri na ikakosolewa sana mitandaoni.

Wakati huo alikana kuwa kwenye mahusiano naye na kusema kuwa uhusiano wake na Samidoh haukuwa wa kimapenzi.

"Samidoh ni rafiki yangu. Nilidhani nilichapisha tu video kama vile unavyochapisha video za marafiki zako wengine. Walakini, watu walianza kutoa maoni tofauti, kama kuhusu mke wa Samidoh, na kwa hivyo niliamua kuifuta. Sikuwa na nia yoyote mbaya, tena Samidoh ni chapa yake mwenyewe, na sikutaka kuichafua. Tulikuwa Dubai ambapo Sonko na wanasiasa wengine walikuwa pia, na tulikuwa tukikaa karibu na eneo moja, na tulipanda mashua pamoja kama marafiki," alisema.

Mwezi Desemba, Karen alitangaza kuachana na mwimbaji huyo baada ya drama iliyojitokeza kwenye tamasha lake jijini Dubai.