Alikiba na aliyekuwa mkewe, Amina Khalef wamsherehekea mtoto wao miezi baada ya talaka

Mwanawe Alikiba, Keyaan Kiba alitimiza miaka minne siku ya Jumamosi.

Muhtasari

•Huku akimsherehekea, Alikiba alimtakia mwanawe maisha marefu na mafanikio makubwa maishani.

•Talaka ya wanandoa hao wa zamani iligonga vichwa vya habari nchini Kenya na Tanzania mapema mwaka jana.

Amina Khalef na Alikiba
Image: HISANI

Mwanawe Alikiba, Keyaan Kiba aliadhimisha siku yake ya kuzaliwa siku ya Jumamosi.

Keyaan ni mtoto wa kwanza wa staa huyo wa Bongo na aliyekuwa mke wake Mkenya, Bi Amina Khalef. Mvulana huyo ambaye kwa sasa anaishi na mama yake nchini Kenya baada ya wazazi wake kutalikiana mwaka jana alitimiza miaka minne siku ya Jumamosi, Februari 19.

Huku akimsherehekea, Alikiba alimtakia mwanawe maisha marefu na mafanikio makubwa maishani.

"Kheri ya siku ya kuzaliwa babaa @keyaanalikiba. ALLAH akujaalie elimu ya dunia na akhera na akujaalie umri mrefu wenye faida," mwimbaji huyo alimwandikia mwanawe kwenye ukurasa wake wa Instagram.

Bi Amina Khalef pia alimtakia kheri ya siku ya kuzaliwa mtoto huyo wake wa kwanza kupitia kwenye ukurasa wake.

Wazazi wenza hao walifunga pingu za maisha mwezi Aprili 2018 na wakabarikiwa na watoto wawili kabla ya kutengana.rasmi mwaka jana.

Talaka ya wanandoa hao wa zamani iligonga vichwa vya habari nchini Kenya na Tanzania mapema mwaka jana.

Ombi la talaka liliwasilishwa mahakamani na Bi Amina Khalef, ambaye ni mchambuzi wa masuala ya fedha.

Miezi kadhaa baadaye, mama huyo wa watoto wawili alitangaza kwamba yupo 'huru rasmi', ujumbe ambao ulieleweka kumaanisha kesi ya talaka na bosi huyo wa King's Music Records  ilikuwa imekamilika.

Amina, ambaye sio maarufu sana kwenye mitandao ya kijamii, alipakia picha ya ngome iliyo wazi na ndege akiruka.

Pia alifuta picha zote na AliKiba, zikiwemo zile za harusi yao ya kifahari iliyofanyika  takriban miaka mitano iliyopita.

Duru za kuaminika sasa zilisema AliKiba alijaribu kuokoa ndoa yake, ingawa mwishowe juhudi zake zikaambulia patupu.

“Tangu alipoomba talaka, Alikiba amesafiri kwenda Kenya mara nyingi akiwa hajitambui ili kujaribu kurekebisha mambo, lakini Amina alionekana kuwa ameamua,” mtu mwenye ufahamu wa yaliyotokea alisema.

Kabla ya kudai talaka, inasemekana Amina alimpa mwimbaji huyo nafasi ya kurekebisha mambo, lakini hakufanya hivyo.

"Amina alikuwa ameamua kutulia na kulea familia na Ali," chanzo kilisema.

"Ilifika wakati alihisi kuwa alikuwa akimchukulia kawaida na hakuweza kuvumilia tena. Aliamua kuondoka."

Mwaka wa 2021, mamake Alikiba alithibitisha kwenye mahojiano kuwa wanandoa hao walikuwa wamechukua mapumziko kutoka kwa kila mmoja.