Kajala ashangazwa na upendo wa mwanadada aliyechora tattoo yake na bintiye, Paula

Mwanadada mmoja alichora majina 'Kajala’ na ‘Paulah' kwenye mgongo wake.

Muhtasari

•Siku ya Jumatatu, Kajala alionyesha picha ya mgongo wa mwanadada huyo wenye majina ‘Kajala’ na ‘Paulah.’

•Haya yanajiri takriban wiki mbili tu baada ya mwanadada mwingine kuchora tattoo ya aliyekuwa mpenzi wake, Harmonize.

Paula na mama yake Kajala Masanja
Image: INSTAGRAM// PAULA KAJALA

Aliyekuwa mpenzi wa mwanamuziki Harmonize, muigizaji Frida Kajala Masanja alizidiwa na hisia baada ya mwanadada mmoja wa Tanzania kuchora tattoo ya jina lake na la  binti yake wa pekee, Paula Paul.

Siku ya Jumatatu, Kajala alionyesha picha ya mgongo wa mwanadada huyo wenye majina ‘Kajala’ na ‘Paulah.’

Muigizaji huyo mkongwe alieleza kuwa alishangazwa na upendo wa mwanadada huyo kwa yeye na bintiye.

"Huu Upendo wako kwetu," aliandika na kuambatanisha na emoji za kuonyesha upendo na kuzidiwa na hisia.

Haya yanajiri takriban wiki mbili tu baada ya mwanadada mwingine kuchora tattoo ya aliyekuwa mpenzi wake, Harmonize.

Mapema mwezi huu, staa huyo wa Bongo alimthamini mwanadada ambaye alichora tattoo ya uso wake kwenye ngozi yake.

Bosi huyo wa Kondegang alionyesha video ya tattoo ya mwanadada huyo na kupongeza upendo wa baadhi ya watu kwake. Hata hivyo, aliweka wazi kwamba hayupo tayari kujaribu mahusiano mapya baada ya kuvunjwa moyo mwishoni mwa mwaka jana.

"Asante kwa hili mpendwa, Mungu akubariki mtoto wa kike. Lakini, niko single!" alisema kwenye video hiyo aliyochapisha Instagram.

Konde Boy alidokeza kwamba ni vigumu kwake kujitosa kwenye mahusiano mengine kwa kuwa imekuwa vigumu kwake kumwamini yeyote.

Aidha, alidokeza kwamba wakati akiwa kwenye mahusiano yake ya awali alidanganywa sana na wapenzi ambao hakuwafichua.

"Kuna wasichana ambao wananipenda kabisa. Ni vigumu sana kwangu kumwamini mtu yeyote TENA!!! Ewe Mungu, NATAKA KUWA SINGLE MILELE . Siwezi kukubali uongo tena," Alisema staa huyo wa Bongo.

Wakati huo huo, mwimbaji huyo alidokeza kwamba alijitoa mali na hali ili kumridhisha mpenzi wake wa zamani.

Kufuatia hilo, hasidi huyo wa Diamond Platnumz aliwashauri wanaume kuzingatia kutengeneza pesa badala ya mapenzi.