Hata nikifa leo, nisingependa anizike au kuniomboleza- Amira afunguka chuki yake kwa Jimal

Amira alidokeza kuhusu ndoto yake kuoelewa tena siku moja.

Muhtasari

•Amira alikiri chuki yake kubwa kwa mzazi huyo mwenzake na kubainisha kuwa daima hatawahi kumsamehe.

•Alibainisha kuwa hajutii kamwe kugura ndoa hiyo na hata akasema kwamba anatamani angeondoka mapema.

Amira na aliyekuwa mumewe, Jamal Rohosafi
Image: INSTAGRAM

Mfanyibiashara mashuhuri wa mapambo Being Amira ameweka wazi kuwa aliyekuwa mume wake, Jimal Marlow Rohosafi ndiye mwanaume mbaya zaidi ambaye amewahi kukutana naye maishani.

Huku akiwashirikisha mashabiki wake katika kipindi cha maswali na majibu kwenye mtandao wa Instagram siku ya Jumapili, Amira alikiri chuki yake kubwa kwa mzazi huyo mwenzake na kubainisha kuwa daima hatawahi kumsamehe.

Mama huyo wa wavulana wawili alibainisha kuwa alivumilia ndoa sumu na mwenyekiti huyo wa muungano wa wamiliki wa matatu jijini Nairobi kwa miaka mingi kwa ajili tu ya ustawi wa watoto wao.

"Nilikaa kwenye ndoa yenye sumu kwa sababu yao, nilishikilia ndoa ambayo tayari ilikuwa imevunjika. Alikuwa mtu mbaya zaidi ambaye nimewahi kukutana naye na ninamchukia sana, sitamsamehe kamwe, na hata kama nitakufa leo (Mungu tu anajua ni lini) nisingependa anizike au hata kuniomboleza,” alisema.

Amira aliweka wazi kuwa kwa sasa ametengana rasmi na baba huyo wa watoto wake wawili na hata kuonyesha barua ya talaka.

Alibainisha kuwa hajutii kamwe kugura ndoa hiyo na hata akasema kwamba anatamani angeondoka mapema.

"Nipo na raha mahali nilipo sasa," alisema.

Mama huyo wa watoto wawili alimshtumu mume huyo wake wa zamani kwa kuwa na fitina ndogo ndogo  na uovu.

Alifichua kwamba suala la ushirikiano katika malezi baina yao baada ya kutengana halijakuwa rahisi hata kidogo.

"Ni mbaya. Ninawapenda watoto wangu hadi kufa na kama ningekuwa na chaguo la kurudi nyuma  na kufanya maamuzi sahihi, nisingemchagua kama baba yao, kwa bahati mbaya maji uliyoyafulia nguo, hakuna budi kuyaogea," alisema.

Ingawa alisusia swali iwapo yupo kwenye mahusiano mengine tayari, Amira alidokeza kuhusu ndoto yake kuoelewa tena siku moja.