Mwanablogu wa YouTube Chebet Rono hatimaye ametoa msamaha baada ya kujaa mitandaoni katika wiki moja iliyopita akiburuzana na watu mbali mbali, haswa wanawake wenzake maarufu katika Sanaa nchini.
Rono kupitia ukurasa wake wa Twitter alifichua kwamba alipokea simu ambayo ilimchuna sikio na kumpa funzo kubwa ambalo lilimfanya kutaka Amani kutoka kwa wote ambao alikuwa amewachafua kwa maneno ya kashifa.
Mtangazaji huyo wa zamani alianza na mwigizaji Kate Actress na Elsa Majimbo kisha baadae akawatupia maneno mtangazaji Kamene Goro na Mwanamuziki Nikita Kering miongoni mwa wanawake wengine maarufu.
Aliwataka wote kumsamehe.
"Samahani kwa yeyote niliyemkosea, nimepigiwa simu ambayo imeniambia ukweli wacha niache nikapona tena naomba msamaha kwa tabia yangu," Rono alisema.
Katika kashifa yake, Rono alianza kutupa maneno kwa Kate Actress akimtuhumu kuwa alikuwa ameiba wazo la maudhui yake ambalo alikuwa amekuja nalo kuhusu shangazi tajiri na kumtaka kukoma.
Hata hivyo, mwanadada aliyejidai kuwa aliwahi kuwa rafiki wake wa karibu alijitokeza akifunguka makubwa kwamba huenda Rono hakuwa sawa akizungumza hivyo bali alikuwa na matatizo ya msongo wa akili.
Rono mwenyewe alipakia klipu ya huyo mwanadada akizungumza na kuweka emoji za kucheka tu bila kusema lolote kuhusu madai ya kusumbuliwa na matatizo ya akili.